NA DENIS MLOWE IRINGA
MWENYEKITI wa Chama cha Mpira Wilaya ya Iringa, Joel Musiba, amesema kuwa chama hicho kimekutana na viongozi wa timu zote zilizochukua fomu za ushiriki wa Ligi ya Wilaya kwa lengo la kukumbushana kanuni na kuweka misingi itakayowaongoza katika msimu ujao wa mashindano.
Akizungumza katika kikao hicho, Musiba amesema wamewaita viongozi wa timu ili washiriki katika kutengeneza na kupitisha kanuni zitakazotumika kwenye ligi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila timu inafuata taratibu za usajili kuanzia ngazi ya wilaya hadi Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Amesisitiza kuwa kanuni hizo zinalenga kudhibiti nidhamu ya viongozi, wachezaji na mashabiki pamoja na kuweka utaratibu wa kushughulikia makosa kwa haki na kwa mujibu wa taratibu watakazojiwekea.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mpira Wilaya ya Iringa, Yahaya Mpelembwa, amesema kikao hicho cha Kamati ya Ligi na vilabu kinafanyika katika uwanja wa Samora kikiwa na malengo makuu matatu: kutambua vilabu vyote vitakavyoshiriki Ligi ya Wilaya, kuwasomea kanuni mpya, na kutoa utaratibu wa uendeshaji wa ligi kwa msimu wa 2026/27.
Amefafanua kuwa hadi sasa vilabu 30 kutoka kata zote 46 za Wilaya ya Iringa ndiyo vithibitisha kushiriki. Vilabu hivyo vinatoka katika majimbo matatu ya Iringa Mjini, Kalenga na Ismani. Mpelembwa ameongeza kuwa licha ya changamoto ya kutopata wadhamini hadi sasa, chama bado kinalazimika kuanza ligi kwa mujibu wa kalenda ya TFF ili kutoa nafasi kwa ligi za mkoa na zile za juu kuendelea bila kukwama.
Amesema gharama za ushiriki katika ligi hiyo zimepangwa kuwa shilingi 120,000, kiwango ambacho ni kidogo kulinganisha na maeneo mengine, ili kutoa nafasi kwa timu nyingi zaidi kushiriki bila vikwazo.
Aidha, ameendelea kutoa wito kwa wadhamini kujitokeza kwani kwa misimu iliyopita ligi imekuwa na ubora na imeonyesha uwezo wa kuzalisha vipaji kwa manufaa ya wilaya na taifa.
Alimalizia kwa kusisitiza kuwa maendeleo ya mpira kitaifa hayawezi kupatikana bila kuwekeza kwenye ngazi za chini.
Amesema dhamira ya chama hicho ni kuhakikisha ndani ya misimu miwili hadi mitatu wanapata timu zitakazopanda hadi daraja la kwanza na hata kufikia Ligi Kuu endapo mipango itaenda kama ilivyopangwa.