‎Na. Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

‎Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka nguvu kubwa katika diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuvutia uwekezaji, kuongeza biashara na kutafuta fursa za maendeleo kwa Watanzania.

‎Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Leo Mei 26, 2026 bungeni Dodoma, Waziri Kombo amebainisha kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Wizara ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kulinda maslahi ya Tanzania duniani pamoja na kuendeleza utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la 2024.

‎Vipaumbele vingine vya wizara ni Kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa, Kulinda taswira, heshima na kutetea maslahi ya Tanzania katika nyanja ya kimataifa, Kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Wizara, kuimarisha utawala bora na rasilimali watu pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo ya Wizara na taasisi zake.

‎Aidha, amesema kuwa Serikali itaendelea kutumia diplomasia ya uchumi kufungua masoko mapya ya bidhaa za Tanzania, kuvutia wawekezaji pamoja na kuongeza fursa za ajira, elimu na teknolojia kupitia ushirikiano wa kimataifa.

‎Pia ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa sambamba na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wake ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.