📍 DODOMA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limewafukuza kazi watumishi watatu na mtumishi mmoja kushushwa cheo na mshahara kufuatia kukiuka misingi na taratibu za Utumishi wa Umma.
Maamuzi hayo yalifanyika katika Mkutano maalum wa Mashauri ya Kinidhamu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Watumishi waliofukuzwa kazi ni Afisa Muuguzi Msaidizi, Muuguzi na Afisa Mtendaji wa Mtaa. Mtumishi aliyeshushwa cheo na mshahara ni Mteknolojia Maabara.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula alilihoji Baraza la Madiwani, na kwa kauli moja liliridhia kuwafukuza kazi watumishi hao watatu na kushushwa cheo na mshahara mtumishi mmoja.
Akiwasilisha taarifa ya kuhitimisha mashauri ya nidhamu ya watumishi wanne kwa Baraza maalum la Mashauri ya Nidhamu, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Gerald Ruzika alisema kuwa mkurugenzi aliunda kamati ya uchunguzi kwa mujibu wa Kanuni ya 45 na 46 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 kuchunguza tuhuma dhidi ya watumishi wanne.
Akiongelea tuhuma hizo, alisema kuwa watumishi wote, kamati ilithibitisha tuhuma walizotuhumiwa nazo kuwa ni za kweli isipokuwa mtumishi wa cheo cha Mteknolojia Maabara ambae kamati haikuthibitisha tuhuma moja ya kufanya mambo yanayoshusha hadhi ya Utumishi wa Umma kinyume na Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, Kanuni ya 42 Jedwali la kwanza sehemu A (2) kati ya tuhuma nne alizotuhumiwa nazo.
Akiongelea mashtaka waliyotuhumiwa nayo alisema kuwa Mteknolojia Maabara alishtakiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa sababu ya matumizi ya pombe yaliyokithiri, kutumia bila idhini ya mamlaka vifaa vya umma kwa shughuli zisizohusiana na majukumu yake, kufanya mambo ambayo yanashusha hadhi ya Utumishi wa Umma, kwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma na kutokuwepo kazini kwa zaidi ya siku tano bila kuwa na likizo ama ruhusa ya mwajiri.
Kwa upande wa Afisa Muuguzi Msaidizi alishtakiwa kwa kutokuwepo kazini kwa zaidi ya siku tano bila kuwa likizo au ruhusa ya mwajiri.
Muuguzi alishtakiwa kwa kutokuwepo kazini kwa zaidi ya siku tano bila kuwa likizo, ruhusa ya mwajiri au sababu za msingi na kutofanya majukumu aliyopangiwa kama mtumishi wa umma.
Mtendaji wa Mtaa alishtakiwa kwa kutokuwepo kazini bila kuwa likizo, ruhusa au sababu za msingi na kutotekeleza majukumu aliyopangiwa kama mtumishi wa umma.

