Na mwandishi wetu Kasulu.

Mnamo tarehe 25.05.2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Kasulu mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya Mhe. S.A.Mchalo (SRM) na Mwendesha Mashtaka kutoka TAKUKURU Bw. Davis Junior limefunguliwa shauri la jinai Namba CC.11343/2026 Jamhuri dhidi ya ELIAS KAZILI BAKIMBAGA (54) ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Kigadye  

Bakimbaga ameshtakiwa katika mahakama hiyo akituhumiwa kwa kosa la kuomba na kupokea hongo kinyume na kufunga cha 15(1) (a) na 15(2) vya PCCA sura ya 329 marejeo ya mwaka 2023,

Ambapo ilielezwa kwamba mnamo tarehe 22.03.2026 Bw. Elias Kazili Bakimbaga anatuhumiwa kumuomba Bi. Helena Juma fedha kiasi cha Tsh.150,000/= ili aweze kumwachia huru mme wake Bwana Mashilimu Kinasa aliyekuwa ameshikiliwa na kufungiwa katika chumba kimoja cha ofisi ya mtendaji wa Kijiji cha Kigadye kwa kosa la kuingia na Kulima katika shamba la mtu mwingine bila ridhaa yake.

Kwamba tarehe 23 Machi 2026 Bw. Elias Kazili Bakimbaga alipokea kutoka kwa Bi. Helena Juma fedha kiasi cha Tsh.130,000/= ili aweze kumwachia huru mme wake Bwana Mashilimu Kinasa aliyekuwa ameshikiliwa na kufungiwa katika chumba kimoja cha ofisi ya mtendaji wa Kijiji cha Kigadye kwa kosa la kuingia na Kulima katika shamba la mtu mwingine bila ridhaa yake fedha za mtego wa Rushwa ulioandaliwa na maafisa wa TAKUKURU Kasulu ambao walimkamata baada ya kuwa amenasa katika mtego huo.

Baada ya kusomewa Mashtaka yake mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo. 

Mshitakiwa ameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya Mahakama.

Shauri limepangwa kusikilizwa tena tarehe 01.06.2026 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali (PH).