Na. Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa Tanzania inaendelea kushikilia sera yake ya kutofungamana na upande wowote katika masuala ya kimataifa huku ikiendeleza ushirikiano na mataifa mbalimbali duniani kwa maslahi ya taifa.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Leo Mei 26,2026 bungeni Jijini Dodoma, Kombo amebainisha kuwa misingi ya sera ya mambo ya nje ya Tanzania imeendelea kuzingatia kulinda mamlaka kamili ya nchi, uhuru wa kisiasa, haki za binadamu, usawa, demokrasia pamoja na kukuza umoja wa Afrika.
Aidha, amesema kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa katika kuimarisha amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi duniani bila kuegemea upande wowote katika migogoro ya kimataifa.
Pia ameongeza kuwa sera hiyo ya kutofungamana imeendelea kuipa Tanzania heshima kubwa duniani na kuifanya kuwa mshirika anayeaminika katika diplomasia ya kimataifa.
Kombo amesema kuwa kupitia sera hiyo, Tanzania imefanikiwa kujenga mahusiano mazuri na mataifa mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa hali inayosaidia kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kulinda maadili, mila na utamaduni wa Watanzania huku ikiimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

