Na, mwandishi wetu – Msumbiji
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi ameupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji kwa namna unavyoendelea kutekeleza majukumu yake na kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea ofisi hizo pamoja na ujumbe alioongozana nao kwa lengo la kushiriki katika ziara ya kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Msumbiji kuhusu hatua za mapema kabla ya majanga unaoendelea kwa siku tano kuanzia tarehe 25 hadi 29 Mei, 2026 Mjini Maputo Msumbiji.
Dkt. Yonazi amezungumza na watumishi wa ubalozi huo na kupokea taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Ubalozi iliyotolewa na Mwambata fedha Bw. Samson Marwa kwa niaba ya Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji ambaye alikuwa katika majukumu mengine.
Aidha, amewashukuru watumishi wa ubalozi huo kwa namna wanavyoendelea kutekeleza majukumu ya msingi huku wakiiwakilisha nchi na kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa vitendo.
“Ninawapongeza namna mnavyoendelea kuiwakilisha nchi yetu, ni vyema kuendelea kuangalia fursa zilizopo na kuzitangaza hususan za kiuchumi zitakazowavutia kuja kuwekeza Tanzania, niwasihi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu,” alisema Dkt. Yonazi
Kwa upande wake Mwambata fedha wa ubalozi huo Bw.Samson Marwa akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kutenga muda wake na kuzitembelea ofisi za ubalozi huku akiahidi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuhakikisha jukumu la msingi la kuhakikisha uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji linaendelea kuimarika kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
“Tunashukuru kwa ziara hii muhimu kwetu, mnapotembelea ofisi zetu za ubalozi inaonesha kujali na kutambua kazi zinazofanywa, tunaahidi kuendeleza diplomasia na kuitangaza nchi yetu na fursa zilizopo Tanzania,” alisema Marwa
Sambamba na hilo alieleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na wa kidugu kati ya Tanzania na Msumbiji huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwa kuzingatia mchango wa Tanzania kwa Taifa hilo.

