Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB), Bw. Juma Mkomi, amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika taasisi za Serikali kushiriki kikao kazi kitakachofanyika Jijini Dodoma kuanzia Juni 1 hadi 3, 2026 kwa lengo la kujadili maboresho ya usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma.
Ameyasema hayo Mei 26,2026 Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari , Aidha, Mkomi amesema kikao hicho kitawakutanisha viongozi kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amesema kikao hicho kitaongozwa na kaulimbiu isemayo “Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Ulio Sikivu, Jumuishi, wenye Matokeo na Uwajibikaji Kuelekea Dira 2050.”
Aidha, Mkomi amebainisha kuwa kikao kazi hicho hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika usimamizi wa rasilimaliwatu.
Ameongeza kuwa kikao hicho kitajadili matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidijitali ikiwemo e-Uhamisho, e-Watumishi, e-Utendaji, e-Mrejesho pamoja na HR Assessment kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Pia amesema washiriki watapata nafasi ya kujadili mafanikio na changamoto zilizopo katika Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu pamoja na kupendekeza njia bora za kukabiliana nazo.
Katika hatua nyingine, Mkomi amesisitiza viongozi wote wenye dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu kushiriki kikao hicho wao wenyewe bila ya kuwakilishwa kutokana na umuhimu wake.
Amebainisha kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete.
Sambamba na hilo, Mkomi amesema washiriki wote wanatakiwa kujisajili kupitia mfumo wa TSMS kwa kutumia tovuti ya [TSMS](https://tsms.gov.go.tz?utm kabla ya Mei 29, 2026 saa 6:00 usiku ili kurahisisha maandalizi ya kikao hicho.

