Wekundu wa Msimbazi Simba SC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo, Mei 24, 2026, kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Simba SC ilipata ushindi huo kupitia kwa Elie Mpanzu dakika ya 63, baada ya Clatous Chama kukosa penalti. Kipa wa Dodoma Jiji FC alitibua mpira huo, lakini ulimkuta Mpanzu ambaye aliutumbukiza wavuni na kuandika bao pekee la mchezo.
Kufuatia ushindi huo, Simba SC imefikisha pointi 58 na kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imecheza michezo 25. Wapinzani wao Young Africans SC wanashika nafasi ya pili kwa pointi 57, huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
