📍SAME.
ZAIDI ya Wakulima 23184 katika skimu za umwagiliaji za Ndungu, Ndungu fidia, Kalemane na Vumba jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro wataenda kunufaika na kilimo hicho baada ya serikali kutoa fedha Bilioni 44.159 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Yongoma linakalohifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji.
Akizungumza jana mara baada ya kutembelea mradi huo na kujionea shughuli zinazoendelea, Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alisema kuwa, Mradi huo ni mkubwa ambapo ukikamilima utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na utaongeza tija ya kukuwa kiuchumi.
Alisema kuwa, kutoka na tija hiyo serikali ya wilaya itahakikisha inaulinda na kuusimamia mradi huo ukamilike kwa wakati pamoja na kuwachukua hatua wale wote watakaokuwa na mpango wa kuhujumu mradi huo.
“Serekali imeleta fedha bilioni 44 ni lazima tuusimamia huku mradi kuhakikisha unaleta tija kwa wananchi wa same na hii ni kazi kubwa imefanywa na Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anna Kilango Malecela anapambana kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo” alisema Kasilda.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, wananchi wa Same mashariki wamepata Mbunge mahiri na kuwataka wananchi kuilinda lulu hiyo kwani yapo majimbo wananchi wao hawamwoni Mbunge.
Kasilda alitumia pia nafasi hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopeleka fedha za maendeleo katika wilaya ya Same.
Aliongeza kuwa, mradi huo utaleta tija kubwa kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao likiwemo zao la biashara la Tangawizi ambapo itawasaidia kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka.
