Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu, amefanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Andrew Lentz, kuhusu kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Marekani.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, huduma za kibalozi, biashara na uwekezaji, usalama, nishati pamoja na utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya maendeleo.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie S. Kanza, ambaye alishiriki katika majadiliano yaliyolenga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha, pande zote mbili zilisisitiza dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na kufanya mazungumzo yenye tija kwa manufaa ya mataifa hayo mawili.