Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore amefanya ziara katika chuo cha REDUEdu kilichopo Rovaniemi nchini Finland ili kujionea maendeleo ya wakufunzi 25 wanaopata mafunzo ya ujuzi wa teknolojia zinazohitajika katika Uchimbaji na Ukuzaji Mnyororo wa Thamani wa Madini chuoni hapo.

Katika ziara yake chuoni hapo aliambatana na baadhi ya viongozi wa menejimenti ya VETA Makoa Makuu, jana tarehe 22 Mei 2026 CPA Kasore, amezungumza na wakufunzi hao na kuwataka pindi watakapo hitimu mafunzo yao na kurejea nchini kuhakikisha wanaleta mabadiliko chanya katika taasisi na taifa.

“Kuja kwetu hapa ni kutaka kuona kile tunachokisimamia watu wetu wanakipata kupitia huu mradi. Ndio maana hata leo tulikuwa na majadiliano na wenzetu REDUEdu na GTK kuona mpangilio wa vipindi ukoje na kwa kiasi gani umetekelezwa na wapi pa kufanya maboresho” amesema Kasore.

Aidha CPA Kasore amewataka wakufunzi hao kupita katika karakana zilizopo chuoni hapo ili kujionea hali ya mpangilio wa vifaa vya kujifunzia lakini pia kuona ni jinsi gani wakufunzi wanatoa mafunzo kwa wanafunzi na kuona kinachotakiwa kubadilika katika utoaji mafunzo na utunzaji wa karakana pindi watakapo rejea katika vituo vyao vya kazi.

“Ninapopita kwenye vyuo huwa natazama vitu vingi. Huwenda umekuja hapa lakini kule umeacha karakana yako haipo katika mpangilio mzuri. Pita huku uone kwanini karakana imewekwa katika mpangilio wa aina hii, kwa kufanya hivyo itasaidia kuona nijinsi gani na sisi tunaweza kuboresha nyumbani na kutoa mafunzo bora yanayoendana na viwango vinavyohitajika katika jamii,” amesema Kasore.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilamali watu na Utawala, Enihart Mahudi amewataka wakufunzi hao kushi kwa kufuata misingi na maadili ya watumishi wa umma wakiwa nchini humo, lakini pia ujuzi wanaoupata wakautumie na kwenda kuboresha eneo la madini na kuwajengea uwezo wakufunzi na wananchi ambao hawajapata fursa ya kupata mafunzo hayo.

“Tumieni nafasi mliyoipata kuuliza na kujifunza zaidi, rai yangu kwenu ni kujifunza kwa bidii na kuendelea kuishi kwa nidhamu na kuilinda heshima ya Serikali na kuiwakilisha nchi yetu vizuri ili kuja kutusaidia kama taasisi na taifa kwa ujumla pindi mtakapo hitimu,” amesema Mahundi.

Kwa upande wake kiongozi wa kundi hilo la wakufunzi, Yona Mwambapa ameishukuru Menejimenti ya VETA kwa kuhakikisha wanafanikisha wakufunzi kupata mafunzo nchini humo.