Na John Walter -Hanang’ 

Wananchi wa Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara wamempongeza Mkuu wa Wilaya hiyo, Almish Hazal, kwa jitihada zake za kusikiliza na kutatua kero zao kupitia utaratibu maalum wa kukutana nao kila Jumatatu na Alhamisi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema utaratibu huo umeleta matumaini mapya kwao kwani umesaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa wakati, hususan migogoro ya ardhi ambayo kwa muda mrefu ilikuwa chanzo cha malalamiko katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Wamesema uwepo wa Mkuu wa Wilaya huyo katika kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja umechangia kupunguza migogoro, kuimarisha maelewano na kurejesha imani ya wananchi kwa mamlaka za serikali katika kushughulikia matatizo yao.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almish Hazal, amesema mafanikio ya utaratibu huo ni makubwa kwani malalamiko kutoka kwa wananchi yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Amesema awali wilaya hiyo ilikuwa na migogoro migumu ya ardhi 15, lakini hadi sasa imebaki migogoro minne tu, ikiwemo mgogoro wa mpaka kati ya mikoa ya Singida na Manyara ambao bado unaendelea kushughulikiwa.

“Kila Jumatatu na Alhamisi nimetenga siku maalum kwa ajili ya kuwasikiliza wananchi kuhusu kero walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Hazal.

Ameongeza kuwa viongozi wa wilaya hiyo wanaendelea kuchapa kazi huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida, akibainisha kuwa kila Ijumaa yeye mwenyewe hufika katika maeneo yenye migogoro ili kujiridhisha hali halisi huku wananchi wakihusishwa katika hatua za utatuzi.

Hazal pia amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuisaidia Hanang’ kwa kupeleka shilingi bilioni 7.08 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa madaraja 12 pamoja na barabara zake, ambapo kazi zinaendelea.

Ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwaletea wananchi wa Hanang’ maendeleo, huku akisisitiza kuwa kero nyingi zinazowasilishwa katika ofisi yake zinahusu migogoro ya ardhi ambayo serikali inaendelea kuipatia ufumbuzi.

Wananchi wa Hanang’ wameeleza kuwa hatua ya Mkuu wa Wilaya huyo ya kusikiliza na kushughulikia kero zao imekuwa chachu ya kupunguza malalamiko na kuimarisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili.