Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa mageuzi ya elimu nchini hayaishii kwenye sera na mitaala pekee bali yanahusisha maeneo mbalimbali muhimu yanayolenga kuboresha sekta hiyo kwa ujumla.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikijikita katika maeneo saba muhimu ambayo ni sera, sheria, mitaala, idadi ya walimu, ubora wa walimu, miundombinu pamoja na vitendea kazi.
Aidha, amebainisha kuwa sera ndiyo msingi mkuu unaotoa mwelekeo wa utekelezaji wa mambo yote katika sekta ya elimu huku sheria zikihitajika ili kuweka misingi ya utekelezaji wa sera hizo.
Ameyasema hayo Mei 22, 2026 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau wa sekta ya elimu kilichokuwa kinajadili mapitio ya Sheria ya Elimu.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu pamoja na kuhakikisha vitendea kazi kama vitabu vinapatikana vya kutosha.
Amesema kuwa kwa sasa elimu ya lazima nchini ni miaka saba, lakini sera mpya inaelekeza elimu ya lazima kuwa miaka kumi hadi kidato cha nne hivyo kuna ulazima wa kufanya mabadiliko ya sheria ili kuendana na utekelezaji wa sera hiyo.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali inakusanya maoni ya wadau ili kuamua kama kutakuwa na marekebisho ya sheria iliyopo ya mwaka 1978 au kutungwa kwa sheria mpya kabisa ya elimu.
Ameongeza kuwa sekta binafsi sasa ina mchango mkubwa katika utoaji wa elimu tofauti na ilivyokuwa mwaka 1978 ambapo taasisi nyingi zilikuwa za Serikali, hivyo wadau hao wanapaswa kutoa uzoefu na mapendekezo yao katika maboresho ya sheria hiyo.
Prof. Mkenda amesema kuwa maoni yatakayokusanywa yatawasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa ajili ya hatua zaidi ikiwemo ushauri kwa Rais kuhusu mwelekeo wa sheria mpya au marekebisho ya sheria iliyopo.
Aidha, amebainisha kuwa nafasi ya Kamishna wa Elimu ni muhimu kwani ndiye mshauri wa kitaalamu katika masuala ya elimu na anapaswa kuwa mtaalamu wa sekta hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir amesema kuwa kikao hicho kimelenga kusikiliza taarifa ya awali ya mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 iliyotayarishwa baada ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.
Amesema kuwa mchakato huo ulioanza mwaka 2024 umechukua muda ili kuhakikisha makundi mengi ya wadau yanashirikishwa kwa lengo la kupata sheria bora itakayodumu kwa vizazi vijavyo.
Aidha, amebainisha kuwa ipo haja ya kuweka rasimu ya sheria hiyo kwenye tovuti ya wizara ili wadau wengi zaidi waweze kuisoma na kutoa maoni yao.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa wizara itaendelea kuyafanyia kazi maoni yote yatakayotolewa na wadau kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu nchini.
Ameongeza kuwa mkutano huo pia ni fursa kwa wadau wa elimu kukutana, kubadilishana mawazo na kujenga ushirikiano utakaosaidia kuboresha utoaji wa elimu nchini.
Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu, Wakili Msomi Bi. Frida Mwela amesema kuwa baada ya vikao vya uhakiki, Kamati itaendelea kukamilisha hatua zinazohusu maandalizi ya rejea ya Kamati ambayo itasaidia katika uandaaji wa rasimu ya Sheria ya Elimu.
Ameongeza kuwa rasimu hiyo itazingatia masuala mahususi yatakayokuwa yamependekezwa na wadau kupitia mchakato wa mapitio ya Sheria hiyo.

