NA FAUZIA MUSSA
JAMII imetakiwa kuchangamkia fursa za ufugaji nyuki na upandaji wa mikoko kama njia muhimu ya kuhifadhi mazingira, kuongeza kipato na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maryam Juma Abdallah, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyoandaliwa kupitia mradi wa Zanzibar Joint Program (ZJP), yaliyofanyika Bumbwini Mafufuni, Wilaya ya Kaskazini B.
Alisema ufugaji wa nyuki umeendelea kuwa miongoni mwa shughuli zinazosaidia uhifadhi wa mazingira sambamba na kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia uzalishaji wa asali na bidhaa nyengine zinazotokana na nyuki.
“Ufugaji wa nyuki si chanzo tu cha kipato, bali ni njia mahsusi ya kuhifadhi mikoko, misitu na rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Maryam.
Alieleza kuwa matumizi ya mizinga ya kisasa ya mbao yameongeza uzalishaji wa asali salama huku yakisaidia kulinda mazingira tofauti na mbinu za zamani zilizokuwa zikichangia uharibifu wa misitu.
Aidha alisema soko la asali linaendelea kukua ndani na nje ya nchi, huku mahitaji ya bidhaa hiyo yakiongezeka kila mwaka, jambo linalowapa wananchi fursa kubwa ya kujiongezea kipato kupitia ufugaji wa nyuki wa kisasa.
Katibu huyo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono programu za uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, akieleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni tano zimetengwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuhami maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Sambamba na hilo, aliipongeza jamii ya Bumbwini kwa kuendelea kushiriki katika upandaji wa mikoko na ufugaji wa nyuki, hatua aliyoisema ina mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa wananchi na kulinda mfumo wa ikolojia wa pwani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Mazingira Duniani (UNEP), Clara Makenya, aliwataka wananchi kuongeza juhudi katika uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji wa mikoko na ufugaji wa nyuki wenye tija.
Aliwahimiza washiriki wa mradi huo kuwa mabalozi wazuri wa elimu waliyoipata ili kusaidia jamii nyengine kuelewa umuhimu wa nyuki katika maisha ya binadamu, mazingira na uzalishaji wa chakula.
Naye Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Tanzania (UNRCO), Susan Ngongi Namondo, alisema mazingira salama yana uhusiano mkubwa na ustawi wa nyuki, akionya kuwa kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi kunaweza kuathiri sekta za kilimo na ufugaji wa nyuki iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ni endelevu, hivyo jamii inapaswa kuweka mbele juhudi za kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya sekta ya kilimo, chakula na maisha ya wananchi kwa ujumla,” alisema Susan.
Mwanachama wa Kamati ya Uhifadhi wa Mazingira Kijiji cha Bumbwini Makoba, Siwema Mshenga Issa, alisema mradi wa ufugaji wa nyuki umeleta mwamko mkubwa wa utunzaji wa mazingira katika kijiji hicho.
Alisema hapo awali wananchi wengi walikuwa wakitumia mikoko kwa ajili ya kuni na mkaa pekee, lakini sasa wameanza kuona thamani ya kiuchumi iliyopo katika ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali.
“Kwa sasa wananchi wengi wanaogopa kukata mikoko kutokana na uwepo wa nyuki katika maeneo hayo. Wamegundua kuwa nyuki wanaweza kuwapatia kipato kikubwa zaidi kuliko uuzaji wa kuni na mkaa,” alisema Siwema.
Aidha alisema jamii inaendelea kuotesha mikoko na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwalinda nyuki ili kuhakikisha shughuli hiyo inaendelea kuwa chanzo endelevu cha mapato.
Wananchi hao waliiomba Serikali pamoja na wadau wa mazingira kuwawezesha zaidi kwa vifaa vya kisasa, mafunzo na mbinu bora za usindikaji wa bidhaa za nyuki ili kuongeza thamani ya mazao yao.
Naye Ofisa wa Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Idara ya Misitu Wizara ya Kilimo, Vuai Mkoko Hassan, alisema nyuki wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula kupitia shughuli ya uchavushaji wa mimea.
Alifafanua kuwa kupungua kwa nyuki kunaweza kuathiri moja kwa moja sekta ya kilimo na uzalishaji wa chakula, kwani mazao mengi hutegemea uchavushaji unaofanywa na wadudu hao.
Aidha aliwataka wakulima kujikita zaidi katika kilimo hai na kupunguza matumizi ya kemikali, akisema kemikali hizo huathiri maisha ya nyuki pamoja na ubora wa asali inayozalishwa.
“Nyuki wanapochukua chembechembe kutoka kwenye mimea iliyowekwa kemikali, huweza kuzalisha asali yenye mabaki ya kemikali ambayo huathiri ubora wa bidhaa hiyo,” alisema Vuai.
Siku ya Nyuki Duniani huadhimishwa ifikapo Mei 20 ya kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Uhifadhi wa Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Taifa Letu.”

