Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya Silent Ocean imetoa semina elekezi kwa wafanyabiashara wa Jiji la Mwanza ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa biashara, uagizaji wa bidhaa pamoja na mbinu bora za usafirishaji wa mizigo kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, amesema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa inayochangia kwa kiwango kikubwa pato la taifa baada ya Dar es Salaam kutokana na ukuaji wa shughuli za biashara.
Mkalipa amesema kuwa ujio wa kampuni hiyo umekuja wakati muafaka wa kuwaunganisha wafanyabiashara na huduma za usafirishaji zenye uhakika, ikiwemo kuwapatia fursa za kusafiri na kununua mizigo kwa urahisi.
“Silent Ocean wamekuja kukutana na wateja wao na kuwaunganishia huduma mbalimbali za usafirishaji na ununuzi wa mizigo. Kampuni hizi zimetusaidia sana katika sekta ya usafirishaji wa mizigo lakini pia zimechangia kutoa ajira kwa vijana,” amesema Mkalipa.
Ameongeza kuwa uwepo wa huduma za uhakika za usafirishaji utawasaidia wafanyabiashara wa Mwanza kupata mizigo yao kwa wakati na ubora unaotarajiwa.
“Unaweza kununua mzigo na kutumia kampuni isiyoeleweka, mzigo ukafika bila ubora uliotarajiwa. Hivyo, huduma hizi zitawarahisishia wafanyabiashara kupata mizigo yao kwa usalama na ubora uleule,” amesema Mkalipa.
Mkalipa amesema mzunguko wa biashara Mkoa wa Mwanza ni mkubwa na kila mfanyabiashara ana nafasi ya kufanikiwa kutokana na uwepo wa masoko mbalimbali ya kibiashara.
Akitolea mfano sekta ya uzalishaji wa mayai, amesema bado kuna fursa kubwa ya uwekezaji kutokana na mahitaji kuwa makubwa kuliko kiwango cha uzalishaji uliopo.
“Kwa mfano Ilemela kuna wazalishaji wakubwa wa mayai, lakini hakuna anayezalisha mayai laki moja kwa siku, wakati mahitaji yanaweza kufikia zaidi ya hayo. Hii inaonyesha bado kuna pengo kubwa la biashara katika maeneo mengi,” amesema.
Kwa upande wake, Anna Emmanuel, Meneja wa Kanda ya Ziwa wa kampuni ya Silent Ocean, amesema semina hiyo imelenga kuwapa wafanyabiashara elimu ya namna ya kukuza biashara zao pamoja na kuelewa taratibu za usafirishaji na uagizaji wa bidhaa.
Naye mfanyabiashara kutoka Geita, Mussa Yohana, amesema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa vizuri namna ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kupata uzoefu kutoka kwa wafanyabiashara wengine kuhusu upatikanaji wa masoko.
“Tumepata elimu ya usafirishaji na uagizaji wa bidhaa, lakini pia uzoefu kutoka kwa wafanyabiashara wengine. Silent Ocean imekuwa kampuni ya uhakika katika huduma za usafirishaji,” amesema.
Kwa upande wake, Fatma Nassoro, mfanyabiashara wa chakula jijini Mwanza, amesema semina hiyo imemfungulia uelewa mpya kuhusu namna ya kuagiza bidhaa kutoka nje.
“Nilikuwa natamani kufuata bidhaa mwenyewe lakini sikuwa najua nianzie wapi Kupitia semina hii nimepata uelewa wa namna ya kuagiza mzigo kutoka nje na ukaweza kunifikia nilipo,” amesema Fatma.

