Na Silivia Amandius
Bukoba, Kagera.
Maadhimisho ya Siku ya Wakala wa Vipimo Duniani yamefanyika leo Mei 20 ambayo uazimishwa Kila mwaka, yakiratibiwa kimataifa nchini France, kitaifa jijini Dodoma na kimkoa katika Manispaa ya Bukoba. Katika Mkoa wa Kagera, maadhimisho hayo yamelenga kutoa elimu kuhusu uhakiki wa upimaji wa gesi, matumizi sahihi ya mizani pamoja na ukaguzi wa vituo vya mafuta ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Vipimo Kagera, Johnstone Japhet, amesema wataalamu wa wakala huo wamefanya ukaguzi wa mitungi ya gesi, mizani na baadhi ya pampu za mafuta katika vituo mbalimbali. Amesema pia wamepokea maoni na malalamiko kutoka kwa wananchi na kuahidi kuyafanyia kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Amesisitiza wananchi kuhakikisha wanapimiwa gesi kwenye mizani yenye stika rasmi za Wakala wa Vipimo na kuwahimiza wamiliki wa magari kushiriki moja kwa moja wakati wa kujaza mafuta ili kujiridhisha na kiwango wanachonunua. Aidha amesema baadhi ya changamoto za udanganyifu bado zipo, hivyo ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kudhibiti vitendo hivyo.
Johnstone Japhet ameongeza kuwa sheria sura namba 340 pamoja na kanuni zake zinatoa adhabu kwa yeyote anayekiuka taratibu za vipimo, ikiwemo kutozwa faini. Pia amewataka wauzaji wa gesi kuhakikisha wanakuwa na mizani katika maeneo yao ya biashara ili kuondoa wasiwasi kwa wateja na kuongeza uwazi katika huduma wanazotoa.
Kwa upande wake, muuzaji wa mitungi ya gesi kutoka Manispaa ya Bukoba, Sylvanus Faustin, ameishukuru Wakala wa Vipimo kwa kutoa elimu hiyo akisema imekuwa msaada mkubwa kwake na kwa wananchi wanaonunua gesi. Amesema amekuwa akipokea maswali mengi kutoka kwa wateja kuhusu kiwango halisi cha gesi kwenye mitungi, hivyo elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kuondoa sintofahamu iliyokuwepo.
Katika sekta ya mafuta, maafisa wa Wakala wa Vipimo wameeleza kuwa ukaguzi wa kawaida hufanyika kila mwaka sambamba na ukaguzi wa kushtukiza. Pampu zinazokidhi viwango huwekewa stika maalum za uhakiki ili kuwaonesha wananchi kuwa zimekaguliwa na kuthibitishwa na wakala huo. Aidha wamebainisha kuwa utoaji wa mafuta ni zoezi shirikishi linalohitaji ushiriki wa mteja na muuzaji ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.

