Bonde la ziwa Victoria linaendelea kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi kiuchumi na kiikolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na mchango wake katika sekta za uvuvi, usafirishaji, kilimo, biashara, utalii, uzalishaji wa nishati pamoja na huduma ya maji kwa mamilioni ya wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Bi.Rose Ambrose amesema wakati wa majadiliano kuhusu maendeleo endelevu ya Bonde la ziwa Victoria, ambapo alieleza kuwa pamoja na umuhimu wa ziwa hilo, bado zipo changamoto mbalimbali ikiwemo uchafuzi wa mazingira, uvuvi haramu, magugu vamizi, ukataji miti, ongezeko la watu pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesisitiza kuwa changamoto hizo zinahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya nchi za ukanda huo pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Ziwa Victoria linaendelea kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na nchi jirani katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya Bonde la Ziwa Victoria yanafikiwa kupitia mshikamano, uwajibikaji wa pamoja na ushirikiano wa kikanda.

