Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Jamhuri ya Kenya nchini, Mhe. Mohamed Ramadhan Ruwange, katika kikao kifupi kilichofanyika kwenye Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kidiplomasia na kusisitiza dhamira yao ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kenya. Aidha, walikubaliana kuendeleza majadiliano ya pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika juhudi za kuimarisha ushirikiano na mahusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Mhe. Kombo amempongeza Mheshimiwa Ruwange kwa uteuzi wake na amemuhakikishia ushirikiano wakati wote atakapokuwa anahudumu hapa nchini.
Naye Mhe. Balozi Ruwange ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano uliopo na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, usafiri wa anga, miundombinu na utalii.
Maeneo mengine ni kilimo, teknolojia ya habari na mawasiliano, ufugaji na uvuvi, elimu, nishati, ulinzi na usalama.

