NA DENIS MLOWE IRINGA 

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ametangaza mbele ya waandishi wa habari kuwa maadhimisho maalumu ya kitaaluma yatafanyika kuanzia tarehe 2 hadi 4 Juni 2026 katika Viwanja vya Bustani ya Manispaa ya Iringa, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.

Maadhimisho haya yameandaliwa na Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE), ambapo Ufunguzi rasmi unatarajiwa kufanyika tarehe 2 Juni 2026 katika eneo hilo la Bustani ya Manispaa.

 

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake,Rc Kheri alisema kuwa Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Harnessing Tanzania’s Minerals Wealth for Renewable Energy, Digital Transformation and Social Security”, ikisisitiza umuhimu wa kutumia utajiri wa madini wa Tanzania katika kukuza nishati jadidifu, mageuzi ya kidijitali na ustawi wa kijamii.

 

Alisema kuwa Kaulimbiu hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia, ubunifu na ushirikiano wa taasisi.

 

Mkuu wa Mkoa amewataka wadau kutoka sekta za umma na binafsi pamoja na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo, ambayo yamekusudia kuchagiza maendeleo kupitia utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia.

 

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kutoa huduma mbalimbali bure kwa wananchi ikiwemo vipimo vya afya, ushauri wa kisaikolojia na biashara, upimaji wa usikivu, ushauri wa lishe, pamoja na uchangiaji damu. 

 

 

Aidha, wananchi watapata fursa ya kusikiliza na kujifunza matokeo ya tafiti mbali mbali zinazofanywa na vyuo vikuu, hususan wataalamu wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, pamoja na kuona miradi iliyozaliwa kutokana na tafiti hizo.

 

Mkuu wa Mkoa ametoa mwito kwa wadau na wafanyabiashara kujitokeza kuonyesha bidhaa na huduma zao, huku akisisitiza umuhimu wa kuwasiliana mapema na waandaaji kwa ajili ya kurahisisha taratibu za ushiriki katika maadhimisho hayo ya siku tatu.

 

Kwa upande wa Chuo Kikuu kishiriki cha Mkwawa kupitia Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu, Dr. Selina Mkimbili, amesema kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwaleta pamoja watafiti, wabunifu, wanajamii na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kujadili namna utafiti unavyoweza kuchangia kutatua changamoto za wananchi wa Iringa na taifa kwa ujumla.

 

Dr. Mkimbili alisema kuwa tafiti zinazofanywa chuoni hapo zimejikita katika maeneo ya kilimo, mazingira, lishe na uchumi, yakilenga kutoa majibu ya kisayansi yatakayoboresha maisha ya wananchi.

 

Utafiti mmoja unaovutia wadau ni ule unaohusu zao la ulanzi, ambalo ni maarufu katika mkoa wa Iringa. 

 

Alisema kuwa Watafiti wa MUCE wamebaini kuwa ulanzi una uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye thamani kama spirit na bidhaa nyingine za ethanol, jambo linaloweza kuongeza kipato cha wakusanyaji na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

 

Dr. Mkimbili alisema kuwa mara nyingi ulanzi hutumika pasipo kuchakatwa, hivyo kuboresha uchakataji wake kutalifanya kuwa zao lenye tija zaidi kwa jamii na linaloweza kuongeza ajira.

 

Tafiti nyingine zitakazowasilishwa zinahusu kilimo cha uyoga, ambapo watafiti wameonyesha njia endelevu za kuzalisha uyoga wenye ubora wa hali ya juu na salama kiafya. Teknolojia hiyo inatarajiwa kuwasaidia wakulima wadogo kuongeza kipato na kuingia kwenye masoko kwa ushindani.

 

Pia kutakuwepo tafiti zinazolenga kuwawezesha wakulima wa nyanya, mahindi na mboga mboga kuongeza uzalishaji, kudhibiti wadudu waharibifu na kuboresha ustahimilivu wa mazao dhidi ya changamoto za tabianchi. Hili limeelezwa kuwa eneo muhimu kwa wakulima wa Iringa ambao wanategemea kilimo kama msingi wa uchumi wao.

 

Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa ulanzi, wakulima, wataalamu wa kilimo, taasisi za maendeleo na wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo ili kujifunza na kupata mbinu mpya za kuboresha shughuli zao.

 

Maadhimisho ya Siku ya Taaluma yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuonesha namna utafiti unavyoweza kuchangia mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia katika mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.