Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuiimarisha Taasisi ya viwango Zanzibar ( ZBS ) ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani katika kuhakikisha ubora wa bidhaa kabla ya kumfikia mtumiaji.

Hayo yamemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abulla katika hafla ya usiku wa tunzo za umahiri za ZBS kwa mwaka 2026 hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.

Amesema katika kutambua umihimu wa viwango vya bidhaa na huduma ndani na nje ya nchi Serikali imeanzisha Taasisi ya viwango kupitia sheria ya viwango ya Zanzibar No. 1 ya mwaka 2011 na kuipa jukumu la kuweka viwango na kuvisimamia, kusimamia ubora wa bidhaa na huduma pamoja na kufanya uchunguzi wa bidhaa kupitia maabara mbali mbali kwa lengo la kuhakikisha usalama na afya ya mtumiaji.

 Mhe. Hemed amesema Serikali tayari imezidua mfumo jumuishi wa kisasa wa kielektroniki unaojulikana kwa jina la ZBS Viwango ili kuweza kuiwezesha taasisi hio kufatilia bidhaa kwa usahihi, kutoa vyeti vya ubora kwa haraka na kuwawezesha wadau kupata taarifa kwa njia ya kidigitali hatua itakayoongeza ufanisi zaidi katika sekta ya viwanda na bishara na kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.

Aidha amefahamisha kuwa, Serikali imedhamiria kujenga jengo la kisasa katika eneo la viwanda la Dunga Zuze litakalokuwa na Maabara 20 za kutolea huduma mbali mbali pamoja na kujengwa Maabara ya kisasa na jengo la utawala katika eneo la Viwanda Chamanangwe Pemba .

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais amewahimiza wazalishaji, wafanya biashara na watoa huduma wote kuendelea kuzingatia viwango vinavyowekwa na Serikali ikizingatiwa kuwa ubora wa bidhaa kwani ndio silaha muhimu ya mafanikio ya kiuchumi.

Aidha amesema ubora wa bidhaa si jambo la hiari bali ni wajibu hivyo ni jukumu la kila mfanya biashara na mtumiaji kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa kitovu cha bidhaa na huduma zenye viwango vya ubora vinavyokubalika Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Hata hivyo amewataka wale wote ambao wametunukiwa tunzo kuendelea kuzalisha na kutoa huduma zenye ubora na zenye viwango paamoja na kutumia ubunifu na teknologia ili kuendana na masoko ya Kitaifa na Kimataifa.

Nae Kaimu Waziri wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ambae pia ni Waziri wa Kazi na Uwekezaji Mhe. Sharif Ali Sharif amesema Taasisi ya viwango Zanzibar ( ZBS) imepiga hatua katika kuhakikisha inaangalia ubora wa bidhaa zote zinazoingia na zinazozalishwa nchi kwa maslahi mapana ya watumiaji na nchi kwa ujumla.

Amesema kuwa serikali imeianzisha Taasisi hio kwa lengo la kuhakikisha inasimamia ubora wa bidhaa zote zinazozalishwa na viwanda vya ndani pamoja na wajasiriamali ziweze kuingia katika soko la ushindani la Kikanda na Kimataifa na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Waziri Sharif amesema katika soko la dunia kumekuwa na ushindani mkubwa kwa wafanya biashara na wajasiriamali hivyo amewataka wafanya biashara kuzalisha bidhaa zenye viwango vya hali ya juu kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na serikali.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa ZBS ndugu YUSSUF MAJID NASSOR amesema katika mchakato wa kuwapata washindi katika masindano ya tunzo hizo ZBS ilipokea maombi 42 kutoka kwa wafanyabiashara mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo wadogo.

Amesema katika kuwapata washindi wa tuzo hizo, kamati mbali mbali zenye wataalamu wa uchumi na maendeleo ya biashara ziliundwa ambazo ziliangalia kwa kina vigezo vya msingi vya mashindano hayo ambavyo ni kuandaa kazi zenye kuzingatia Ubunifu, Ubora, Maudhui, Uwasilishaji, athari kwa jamii pamoja na kuzingaia maadili ya taaluma.