………….
NA DENIS MLOWE, IRINGA
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa imethibitisha rasmi kuwa mkoa huo utakuwa mwenyeji wa mashindano ya kitaifa ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2026, ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo tangu kuanza kwa uenyekiti huo mwaka 2025.
Akizungumza na vyombo vya habari, mkuu wa mkoa wa Iringa, Kheri James amesema kuwa mashindano ya ngazi ya shule za msingi (UMITASHUMTA) yataanza tarehe 7 Juni 2026, yakifuatiwa na mashindano ya shule za sekondari (UMISSETA), ambapo kwa ujumla michezo yote itahitimishwa tarehe 30 Juni 2026.
Rc Kheri alisema kuwa Mkoa wa Iringa unatarajia kupokea zaidi ya wanamichezo 7,000 pamoja na viongozi takribani 800 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema kuwa idadi hiyo kubwa ya wageni inatarajiwa kugusa maeneo mengi ya utoaji huduma ikiwemo malazi, chakula, afya, usafiri na utalii hivyo kuwa na faida kwa mkoa wa Iringa.
“Uongozi wa mkoa umesisitiza kuwa kupokea ugeni mkubwa kama huo ni fursa adhimu ya kiuchumi kwa wakazi wa Iringa, kwani mahitaji ya wageni hao yataongeza mzunguko wa fedha katika biashara mbalimbali”
Hivyo Rc Kheri alisema kuwa wananchi na watoa huduma amewataka kujiandaa kikamilifu ili kutoa huduma bora zitakazokuza hadhi ya Mkoa wa Iringa.
Aidha, vyombo vya ulinzi na usalama vimeelekezwa kuimarisha ulinzi kipindi chote cha mashindano kwa kushirikiana na waandaaji. Wananchi pia wametakiwa kuendeleza ushirikiano na kuhakikisha mkoa unakuwa salama kwa wanamichezo na wageni wote.
Kheri amewakaribisha wageni wote kuwa mkoa wa Iringa uko salama na uko tayari kwa ajili ya wanamichezo wa UMITASHUMTA na UMISSETA, viongozi na wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuongeza kuwa wananchi wanatakiwa kujitokeza katika mashindano hayo, huku wananchi wa Iringa wakihimizwa kutumia nafasi hiyo kujiburudisha na kuzitumia fursa za kiuchumi zitakazojitokeza wakati wa mashindano.
Kwa upande wake afisa utamaduni mkoa wa Iringa, Steve Sanga alisema kuwa mkoa wa Iringa umeendelea kujiimarisha katika maandalizi ya mashindano ya kitaifa ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka 2026 huku ukiwa tayari umekamilisha mashindano ya ngazi ya mkoa na kuingia katika hatua ya kambi za maandalizi kwa timu za shule za msingi na sekondari.
Alisema kuwa Hivi sasa wanamichezo wa Iringa wapo kambini wakijiandaa kikamilifu kwa michuano hiyo mikubwa.
Kambi ya mazoezi kwa timu zote inaendelea katika Shule ya Sekondari ya Kleruu ambako ratiba ya mafunzo na masomo imepangiliwa kwa umakini ili kuhakikisha vijana wanajiandaa kimwili na kitaaluma.
Alisema kuwa Kwa upande wa UMITASHUMTA, Iringa imepokea jumla ya vijana 160 wanaoendelea na mazoezi. Baada ya mchujo kukamilika, idadi hiyo itapungua na kubakia 120 watakaosajiliwa kwa ajili ya mashindano ya kitaifa.
Kwa upande wa UMISSETA, timu ya sekondari imepokea takribani 165 wa michezo mbalimbali. Baada ya mchakato wa mchujo na maandalizi, mkoa unatarajia kubakiwa na takribani 120 watakaounda timu rasmi kwa ajili ya mashindano ya taifa.
Sanga alisema kuwa lengo la maandalizi haya makini ni kuhakikisha Iringa inapeleka timu imara, yenye nidhamu, uwezo na ushindani mkubwa kwenye mashindano ya kitaifa.
Kupitia maandalizi haya, Iringa inatarajia kufanya vizuri katika michezo yote na kuendeleza rekodi nzuri ya uwakilishi katika mashindano ya kitaifa.