Paris, Ufaransa

Banda la Tanzania limekuwa moja ya vivutio vikubwa katika ufunguzi rasmi wa Wiki ya Afrika unaofanyika katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa, ambapo wageni mbalimbali wa kimataifa walijitokeza kujionea urithi, utamaduni na vivutio vya Tanzania.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa H. E Thérèse Kayikwamba-Wagner, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Francophonie wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye alitembelea banda la Tanzania na kupata maelezo kuhusu urithi wa Tanzania, mfumo wa jadi wa uchotaji na uhifadhi wa maji pamoja na fursa mbalimbali za utalii nchini.

Katika banda hilo, Tanzania pia ilionesha utajiri wake wa vyakula vya asili ambapo wageni walipata fursa ya kufurahia pilau, mishikaki, mihogo, kachumbari pamoja na vyakula vingine vya Kitanzania vilivyovutia wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi kadhaa za Afrika, viongozi wa UNESCO, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Ufaransa pamoja na wanajamii wa diaspora wa Afrika wanaoishi nchini humo.

Akizungumza pembezoni mwa hafla hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu UNESCO, Mheshimiwa Saidi Yakubu, amesema ushiriki wa Tanzania katika Wiki ya Afrika ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia urithi wa utamaduni, utalii, vyakula vya asili na diplomasia ya utamaduni.

Aidha, wageni wengi waliotembelea banda la Tanzania walionesha kuvutiwa na namna Tanzania ilivyowasilisha kwa ubunifu urithi wake wa kipekee, jambo lililolifanya banda hilo kuwa moja ya maeneo yaliyokuwa na mvuto mkubwa katika maonesho hayo ya kimataifa.

Wiki ya Afrika ni jukwaa muhimu linalozikutanisha nchi za Afrika katika UNESCO kwa lengo la kuonesha mchango wa bara hilo katika utamaduni, elimu, sayansi na maendeleo ya jamii duniani.