📍Njombe

Serikali imetangaza kuwa Mkoa wa Njombe unatarajiwa kuwa kitovu kipya cha uwekezaji wa madini nchini baada ya kugunduliwa kwa madini adimu ya Rare Earth Elements (REE) ya aina mbili ambayo ni Neodymium Nd na Praseodymium Pr yenye mahitaji makubwa katika teknolojia za kisasa duniani.

Akizungumza katika kijiji cha Mkiu Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Lucas Mlekwa, amesema utafiti wa madini hayo unaendelea kufanywa na kampuni ya Hongji Mining Co. Ltd kwa kushirikiana na wazawa, huku soko kubwa la madini hayo likiwa nchini China kutokana na ukuaji wa haraka wa sekta ya viwanda na teknolojia.

Amesema madini ya REE yanatumika katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo pamoja na vifaa mbalimbali vya kielektroniki vinavyotumika duniani kote.

“Mkoa wa Njombe unaendelea kufungua ukurasa mpya wa maendeleo kupitia rasilimali hizi muhimu ambazo zina mchango mkubwa katika mapinduzi ya teknolojia ya kijani duniani,” amesema Mhandisi Mlekwa.

Ameeleza kuwa kampuni hiyo tayari imekamilisha awamu ya kwanza ya utafiti na sasa ipo katika awamu ya pili ya uchunguzi wa kina kabla ya kuanza uzalishaji rasmi katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 280.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mlekwa, zaidi ya shilingi bilioni moja tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo, huku tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) ikiwa katika hatua za mwisho kukamilishwa kabla ya shughuli za uzalishaji kuanza.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Hongji Mining Co. Ltd, Yahya Mohamed, amesema kampuni imechagua kutumia teknolojia ya In Situ Leaching ambayo inapunguza athari kwa mazingira kwa kutohusisha uchimbaji mkubwa wa mashimo ya wazi wala migodi ya chini ya ardhi.

Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yatawezesha uchimbaji endelevu huku yakilinda mazingira na jamii zinazozunguka eneo la mradi.

“Tunataka kuona wananchi wa Njombe wanakuwa sehemu ya mafanikio ya mradi huu kupitia ajira, fursa za biashara na ongezeko la mapato ya kiuchumi,” amesema Mohamed.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Mkoa wa Njombe, kuchochea uwekezaji mpya pamoja na kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na soko la kimataifa la madini adimu ambalo linaendelea kukua kwa kasi duniani.