Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bi. Rose Ambrose, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo, taasisi mbalimbali na wananchi kuwekeza katika uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji za Ziwa Victoria ili kuhakikisha ziwa hilo linaendelea kuwa chanzo cha maisha na maendeleo kwa mamilioni ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Bi. Rose amesema hayo Mei 19, 2026 wakati akifungua Kikao cha Wadau wa Bonde la Ziwa Victoria kinachofanyika katika Hoteli ya Malaika Beach Resort jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kwanza ya siku ya Ziwa Victoria (Lake Victoria Day) yatakayofikia kilele Mei 21, 2026 katika Viwanja vya Nane Nane Nyamhongolo.

Amesema changamoto za maji duniani ikiwemo ukame, mafuriko, uchafuzi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kuathiri jamii na kuvuka mipaka ya kiutawala hivyo zinahitaji ushirikiano wa pamoja, uwekezaji na mshikamano katika kuzitatua.

Bi Rose alisema Maji yanalazimisha jamii kuungana na kushirikiana huku akizialika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, washirika wa maendeleo, watafiti, wanataaluma, asasi za kiraia na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika juhudi za kulinda na kuhifadhi Ziwa Victoria.

Kupitia kikao hicho, wadau wanajadili masuala mbalimbali ikiwemo usalama wa maji, uchumi wa buluu, usafiri wa majini, uvuvi, biashara, uwekezaji pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za Ziwa Victoria kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.

Maadhimisho hayo yameambatana na kauli mbiu isemayo “Maji Yetu, Mustakabali Wetu: Tuungane kwa Usimamizi Endelevu wa Bonde la Ziwa Victoria” inaendelea kuhimiza mshikamano wa kikanda katika kulinda rasilimali za pamoja.