Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Saidi Shaibu Mussa, ametembelea eneo la Nanenane jijini Mwanza kwa ajili ya kujionea maendeleo ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yatakayofanyika Mei 21, 2026.
Ziara hiyo imelenga kukagua na kufuatilia hatua za maandalizi ya tukio hilo muhimu la kimkakati linalotarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo wa kimataifa wanaojihusisha na masuala ya mazingira na uhifadhi wa Ziwa Victoria.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Balozi Mussa amesisitiza umuhimu wa maandalizi kufanyika kwa weledi, ushirikiano na ufanisi ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanakuwa yenye mafanikio makubwa na yenye tija kwa jamii za Bonde la Ziwa Victoria. Amesema tukio hilo ni jukwaa muhimu la kuimarisha uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za ziwa hilo.
Ameongeza kuwa Ziwa Victoria ni rasilimali ya kimkakati inayochangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa kiuchumi na kijamii katika Ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo linapaswa kulindwa na kusimamiwa kwa uendelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Ikumbukwe kuwa Siku ya Ziwa Victoria imeanzishwa kufuatia azimio la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), ambapo Mei 21 ya kila mwaka itakuwa siku maalum ya kutambua mchango wa ziwa hilo kwa nchi wanachama pamoja na kuhamasisha juhudi za pamoja katika uhifadhi wa mazingira yake.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili namna bora ya kuhifadhi mazingira ya Ziwa Victoria pamoja na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwa maendeleo ya jamii zinazolizunguka ziwa hilo.

