Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mkuranga imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Mwandege kwa mfumo wa ghorofa tatu, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi sambamba na kutekeleza sera ya matumizi bora ya ardhi na agizo la Rais kuhusu ujenzi wa majengo kwenda juu.

Mradi huo uliopo Kata ya Mwandege ulikaguliwa na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo .

Mhandisi wa Halmashauri ya Mkuranga, Nisha Nassoro, alisema mradi huo wenye gharama ya Sh bilioni 2.623 umefikia asilimia 81 ya utekelezaji na unahusisha ujenzi wa vyumba 18 vya madarasa pamoja na matundu 42 ya vyoo, ambapo utakamilika ukiwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi zaidi ya 800.

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Awali na Msingi Mkuranga, Jessy Mpangala, shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 3118 wa elimu ya awali na msingi huku ikiwa na madarasa 17 pekee, hali inayosababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani.

Alisema shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa madarasa 51 kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi ukilinganisha na miundombinu iliyopo sasa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, alieleza kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya mradi huo huku akizitaka halmashauri kulinda maeneo ya taasisi za umma kwa kuyapima na kuyapatia hati ili kudhibiti vitendo vya uvamizi na uuzaji holela wa ardhi.

Alidai baadhi ya watumishi na watendaji wa serikali wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kujinufaisha kupitia uuzaji wa ardhi za taasisi za umma kinyume cha utaratibu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amepongeza halmashauri kujenga shule kwa mfumo wa ghorofa akieleza kuwa ni njia sahihi ya kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa maeneo na kuboresha mandhari ya miji.

“Upande wa elimu tupo vizuri, tumeanza kujenga majengo ya aina hiyo na kutumia teknolojia ya madarasa janja kwa lengo la kuweka rekodi mpya kupitia sekta ya elimu,” alifafanua Kunenge.

Katika ziara hiyo, kamati hiyo pia ilipitia mradi wa kituo cha kupoozea umeme Mbezi-Msufini na mradi wa ujenzi wa ukumbi wa kisasa, ofisi na hoteli Mkuranga unaotekelezwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.