Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini sambamba na kuhakikisha huduma hizo zinadhibitiwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo usafiri wa anga.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/27, ambapo alieleza kuwa TMA imeendelea kutoa huduma za hali ya hewa kwa lengo la kuongeza usalama, ufanisi na uhakika wa shughuli za usafiri pamoja na sekta nyingine zinazotegemea taarifa za hali ya hewa.
Amesema katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa sekta ndogo ya usafiri wa anga, TMA imefanikiwa kukamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Mpanda na Pemba, hatua ambayo inalenga kuongeza ubora wa taarifa za hali ya hewa kwa marubani na wadau wa usafiri wa anga.
Aidha, Profesa Mbarawa amesema TMA inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya hali ya hewa ikiwemo maabara ya uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa (Calibration Center) inayojengwa jijini Dar es Salaam, ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 46.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya hali ya hewa ili kuimarisha uwezo wa utoaji wa taarifa sahihi na za wakati, hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza usalama katika sekta ya usafiri na shughuli nyingine za kiuchumi nchini.
