Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa amesema Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania imeendelea kuimarisha huduma za usafiri wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma, hatua iliyochangia ongezeko kubwa la idadi ya abiria wanaotumia huduma hiyo.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi bungeni, Profesa Mbarawa amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya abiria milioni 2.51 walisafirishwa kupitia reli hiyo ikilinganishwa na abiria milioni 2.05 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 22.4, jambo linaloonesha kuendelea kuimarika kwa huduma za usafiri wa SGR pamoja na kuongezeka kwa imani ya wananchi katika matumizi ya reli hiyo ya kisasa.

Aidha, Profesa Mbarawa amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, TRC ilisafirisha jumla ya tani 102,452 za mizigo kupitia reli ya SGR ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuanza rasmi huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa kutumia reli hiyo.

Amesema mafanikio hayo yanaendelea kuonesha mchango wa mradi wa SGR katika kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji nchini pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi.