Ujumbe wa Baraza la Biashara la Saudi Arabia na Tanzania (Saudi-Tanzania Business Council), Agosti 18, 2026, umetembelea Ofisi za Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujionea utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt. Venanсe Mwasse, amesema Shirika hilo lina wajibu wa kuweka mikakati katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini, kuanzia utafiti, uchimbaji, uchakataji hadi uuzaji wa madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza hilo, Mhandisi Abdulrahman Al-Thubaiti, ameipongeza STAMICO kwa kazi nzuri inayofanyika na kusema ziara hiyo imewapa fursa ya kufahamu zaidi kuhusu uwekezaji na sera zinazohusu sekta ya madini nchini.

Aidha, ujumbe huo umetembelea eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutathmini fursa mbalimbali za uwekezaji.

Ujumbe huo upo nchini kwa ziara ya siku tano yenye lengo la kuibua fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Saudi Arabia na Tanzania katika sekta za kimkakati, ikiwemo madini, kilimo, nishati na viwanda.