Na John Walter -Babati
Wasanii maarufu nchini Dully Sykes, Banana Zoro na Mr Blue wanatarajiwa kutumbuiza kwenye mbio za Manyara Tanzanite Marathon 2026, baada ya kuwezeshwa na Mati Super Brands Ltd kupitia kinywaji chake cha Tanzanite Royal Gin kushiriki katika tukio hilo kubwa la michezo na kijamii.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amewakabidhi wasanii hao T-shirt rasmi za marathon hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Agosti 22, 2026 katika Mji wa Babati.
Manyara Tanzanite Marathon imebeba kaulimbiu “Hatua moja okoa maisha”, ikiwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa wodi maalumu ya watoto njiti wanaozaliwa kabla ya wakati, ili kuongeza uwezo wa kuwahudumia watoto hao na kusaidia kuokoa maisha yao.
Ujio wa Dully Sykes, Banana Zoro na Mr Blue unatarajiwa kuongeza hamasa kwa wanariadha, vikundi vya jogging na wananchi watakaoshiriki au kushuhudia marathon hiyo, huku burudani ikiwa sehemu ya kulifanya tukio hilo kuwa jukwaa la kuunganisha jamii katika kuchangia jambo lenye umuhimu kwa watoto njiti.
Mchango wa Mati Super Brands Ltd, kupitia Tanzanite Royal Gin, unaongeza nguvu ya ushiriki wa sekta binafsi katika kufanikisha marathon hiyo, ambayo inalenga kuunganisha michezo, burudani na juhudi za kijamii katika kufanikisha ujenzi wa wodi hiyo maalumu.

