Na Clement Robert, WAF – Dodoma
Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameendelea kuipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi na uboreshaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambao umetajwa kuwa hatua ya kihistoria katika kuimarisha huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.
Akizungumza leo Mei 9, 2026 jijini Dodoma wakati wa semina ya wabunge, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali inalenga kuongeza uwezo wa utoaji huduma kupitia ujenzi wa hospitali ya kisasa itakayowezesha zaidi ya wataalam 4,000 kufanya kazi katika mazingira bora, salama na yenye ufanisi mkubwa.
Mhe. Mchengerwa amesema licha ya Serikali kuendelea kujenga hospitali mpya kwenye maeneo mbalimbali nchini, Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kuwa mhimili muhimu wa huduma za afya, mafunzo ya wataalam pamoja na maendeleo ya sekta ya afya kwa ujumla.
“Kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za matibabu pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo ya zamani ni miongoni mwa sababu zilizoifanya Serikali kuamua kuendeleza mradi huo mkubwa wa maboresho”, amenukuliwa Mhe. Mchengerwa.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Tanga, Mhe. Kasimu Amari Mbaraka, amepongeza juhudi za Serikali akisema kuwa uwepo wa hospitali kubwa ya taifa yenye viwango vya kimataifa ni jambo muhimu kwa maendeleo ya taifa. Aidha, ameishauri Serikali kupanua eneo la hospitali hiyo hadi maeneo ya Jangwani ili iweze kufanana na hospitali kubwa za kimataifa, kama Apollo ya nchini India.
Mbunge huyo pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika kinga dhidi ya magonjwa badala ya kutegemea mfumo wa bima pekee. Amesema utoaji wa elimu ya lishe bora kwa wananchi unaweza kusaidia kupunguza ongezeko la magonjwa pamoja na gharama za matibabu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Morogoro, Mhe. Josephine Kapoma, amepongeza utekelezaji wa mradi huo huku akiishauri Serikali kuhakikisha hospitali za kisasa zinaendelea kujengwa kwenye kila mkoa ili kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi.
Naye Mbunge wa Manyara amesema Serikali kwa hatua hiyo, huku akiitaka izingatie uwepo wa njia mbadala za kupitisha magari katika utekelezaji wa mradi wa Bonde la Msimbazi ili kurahisisha wananchi kufika hospitalini bila changamoto za miundombinu.
Akitoa takwimu za huduma zinazotolewa na hospitali hiyo, Waziri Mchengerwa amesema mwaka 2025 pekee Hospitali ya Taifa Muhimbili ilihudumia wananchi 44,549 waliolazwa pamoja na wakiwepo wa nje 458,474. Aidha, hospitali hiyo hutumia kati ya shilingi bilioni sita (6) hadi nane (8) kila mwaka kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya miundombinu pamoja na vifaa tiba.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuchukua miaka mitano kwa gharama ya dola za Marekani milioni 468.4, sawa na takribani shilingi trilioni 1.2. Fedha hizo zinatokana kwa kiasi kikubwa na mkopo kutoka Korea Kusini, huku Serikali ya Tanzania ikigharamia kodi, maandalizi ya eneo la mradi pamoja na matumizi mengine muhimu.
Serikali, imesema mradi huo utakuwa na ukubwa wa mita za mraba 115,000, hatua inayotajwa kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi zinazotekeleza miradi mikubwa ya hospitali za kisasa kwa gharama nafuu ikilinganishwa na mataifa mengine yenye mifumo mikubwa ya afya duniani.

