NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,amesema CCM inaendelea na mazungumzo juu ya Serikali ya Umoja wa kitaifa(SUK) na kwamba itaweka mbele maslahi ya CCM na nchi na haipo tayari kuburuzwa na kufuata matakwa ya ACT-Wazalendo.
Dk.Mwinyi,ameweka wazi kuwa mazungumzo yanayoendelea kati ya vyama hivyo viwili juu ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja yanazingatia maslahi na matakwa ya CCM kwani ndio Chama kinachoongoza nchi ambacho kimeshinda kihalali kupitia uchaguzi mkuu wa dola uliopita.
Hayo ameyasema katika ziara yake ya kuimarisha uhai wa Chama cha Mapinduzi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja Kichama katika ukumbi wa Ofisi ya CCM huo huko Mahonda
Dk.Mwinyi,alifafanua kuwa CCM inaheshimu mfumo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa ambao upo kikatiba na kisheria na kwamba mazungumzo na maridhiano yoyote yatakayofikiwa yatakayofanyika kwa mujibu wa sheria za nchi.
Katika maelezo yake Dk.Mwinyi,alisema baada ya kumalizika uchaguzi Mkuu wa dola mwaka 2025,kisheria ACT-Wazalendo walitakiwa kuwasilisha majina ya viongozi wanaopendekezwa kuteuliwa nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar pamoja na majina manne ya mawaziri lakini ACT-Wazalendo mpaka sasa hawajawasilisha badala yake walidai wana malalamiko na mapendekezo yao.
“Wanachama wenzangu wa CCM msiwe na hofu juu ya mazungumzo yanayoendelea kwani tunazingatia na kuweka mbele maslahi ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali kwa ujumla,hatuwezi kukubali kuburuzwa na hao ACT-Wazalendo wakitaka kuleta majina sawa na wasipoleta sawa na Serikali itaendelea kuchapa kazi bila wao”,alisisitiza Dk.Mwinyi.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuwashukru wanachama na wananchi wa Mkoa huo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuiletea ushindi CCM na ikashika dola kupitia uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 uliopita.
Alisema ushindi huo ni mkubwa na umefanyika kwa amani hali iliyopelekea Zanzibar kuandika historia kubwa duniani kwa mara ya kwanza uchaguzi mkuu wa dola kufanyika kwa amani na utulivu bila kuwepo na vitendo vya kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
Amesema licha ya ushindi huo ni muhimu kujitathmini kujua mafanikio na changamoto ili kuhakikisha CCM kuwa imara ambapo Kuna mambo matano ya msingi ambayo ni uhai wa Chama,uhai wa wanachama,kuacha makundi,ulipaji wa ada,kuimarisha siasa na uchumi,utekelezaji wa ilani,umoja katika Chama.
Uhai wa Chama na Wanachama
Makamu Mwenyekiti huyo Dk.Mwinyi,amefafanua kuwa suala la uhai wa Chama ni muhimu kwani linaendeleza mshikamano na kuwajengea wananchi imani ya kuendelea kuiamini Serikali na Chama cha Mapinduzi.
Dk.Mwinyi,alifafanua kuwa wanachama wakijua wajibu wao na kupewa masomo ya darasa la itikadi ili kujua wajibu na haki zao ndani ya Chama ili waweze kuongeza hamasa hali inayosaidia wanachama kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika kila uchaguzi Mkuu wa dola na chaguzi zingine nchini.
Makundi ndani ya Chama
Dk.Mwinyi,kupitia mkutano huo alisema kuwa makundi ni jambo la kawaida katika kusaka uonvozi wakati wa uchaguzi lakini Kuna makundi ya baadhi ya watu ndani ya chama hicho yanasababisha migogoro isiyoisha.
Makamu Mwenyekiti huyo,aliwasihi wanachama na viongozi kuachana na makundi yasiyofaha na kutengeneza kundi Moja la CCM ili kujiandaa na uchaguzi Mkuu wa Chama mwaka 2027,kuelekea uchaguzi Mkuu wa dola wa mwaka 2030.
Dk.Mwinyi,alisema kuwa makundi mengi yanaanzishaa na baadhi ya viongozi hasa wawakilishi na wabunge kwa kulimda maslahi Yao binafsi jambo ambalo ni hatari katika uhai wa Chama na kwamba viongozi hao waache tabia hiyo.
Ulipaji wa ada
Dk.Mwinyi alisema suala la kulipa ada ni muhimu kwani linaongeza hamasa na uhalali wa wanachama na kwamba suala hilo lisimamiwe kikamilifu na viongozi husika.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi,alisema ili Chama Cha Mapinduzi kiendelee kuimarika ni muhimu kuweka kipaumbele cha kujiimarisha kiuchumi kupitia rasilimali zake kwa kufanya uwekezaji mkubwa utakaowesha upatikanaji wa fedha nyingi za kuendesha chama hicho.
Dk.Mwinyi,alitoa mfano kuwa CCM ina maeneo mengi ya wazi katika ngazi mbalimbali ambayo hayafanyiwi uwekezaji wenye tija hali inayosababisha Chama kukosa mapato kutokana na kutotumiwa ipasavyo maeneo hayo.
“ Nachukua nafasi hii kuwasihi viongozi wa ngazi mbalimbali kuweni wabunifu kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinanufaika na rasilimali za viwanja vya wazi,majengo na maeneo mengine ya uwekezaji anzisheni miradi mikubwa ili tuingine fedha za kuendesha shughuli mbalimbali za kichama”, alisema Dk.Mwinyi.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
Dk.Mwinyi,alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kinaendelea kutekeleza kwa ufanisi Ilani yake kwa kuimarisha sekta mbalimbali za afya,elimu,maji safi na salama,umeme,barabara za kisasa,sekta ya usafiri wa baharini,usafiri wa anga,ujenzi wa bandari za kisasa,uwekezaji wa miradi mikubwa yenye tija katika ukuaji wa uchumi wan chi.
Alisema katika kutekeleza Ilani hiyo ya 2025/2030 Serikali imejipanga kujenga miundombinu ya kisasa ikiwemo barabara kubwa na viwanja vya kisasa vya michezo vyenye viwango vya kimataifa ili kuendelea kubadilisha maisha ya wananchi wote bila ubaguzi.
Alieleza kuwa CCM ikitoa ahadi inatekeleza kwa vitendo tofauti na vyama vingine ndio maana imeongeza mshahara kutoka 300,000 hadi 500,000 kutokana na ukuaji wa uchumi wan chi.
“Tukiahidi tunatekeleza kwa vitendo ndio maana tuna ilani ya Uchaguzi sio kama wale wenzetu wanatoa ahadi za uongo zisizokuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi wa visiwa hivi vya Zanzibar “, alieleza Dk.Mwinyi.
Akitoa Salamu za Chama Cha Mapinduzi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, alisema ziara hiyo ya Dk.Mwinyi ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi katika kusimamia misingi ya umoja, uwajibikaji,kusikiliza na kuwashukru wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla.
Dkt.Dimwa,alieleza kuwa Zanzibar inaendelea kuimarika kiuchumi,kisiasa na kijamii kutokana na utendaji madhubuti wa Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi toka ameingia madarakani ameweza kufanya kazi kubwa ya kuijenga Zanzibar mpya.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Idd Ali Ame,amesema Mkoa huo umeendelea kuimarika kimaendeleo na wanajivunia kazi kubwa inayofanywa na Serikali chini ya usimamizi imara wa Rais wa Zanzibar Dk.Hussin Ali Mwingi.
Alisema kuwa katika sekta ya elimu Mkoa huo una zaidi ya skuli za ghorofa saba za sekondari na msingi pia vituo vipya vya mafunzo ya amali vinavyowawezesha watoto na vijana wanapata huduma bora za kielimu ndani ya Mkoa huo.
Ame,alieleza kuwa Serikali imetafuta ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ambapo wananchi wanapata huduma ya maji katika makaazi Yao.
Pia alisema kupitia juhudi kubwa za Dk.Mwinyi,Serikali imeimarisha mtandao wa barabara za kisasa zinazorahisisha usafiri kwa wananchi na kuimarisha sekta ya utalii na bandari za kisasa za Mwangapwani mkoani humo.

