NA DENIS MLOWE -IRINGA 

MKUU wa Mkoa wa Iringa amesema mazungumzo yanapaswa kuwa njia kuu ya kutatua changamoto za kikodi ili kulinda mazingira bora ya biashara na kuhakikisha wananchi hawaathiriki kutokana na migogoro kati ya mamlaka na walipakodi.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha matembezi ya shukrani ya maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mkuu wa Mkoa alisema Iringa imejenga sifa ya kuwa na ushirikiano mzuri kati ya wafanyabiashara na TRA, hali iliyochangia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuimarisha uwekezaji.

Alisisitiza kuwa hatua za kusimamisha huduma au kufunga biashara kutokana na migogoro ya kikodi zinapaswa kuepukwa pale inapowezekana, akieleza kuwa meza za mazungumzo na taratibu za kisheria zinatosha kutatua tofauti bila kuwaumiza wananchi wanaotegemea huduma hizo

Kheri aliwapongeza walipakodi kwa uzalendo wao wa kuchangia maendeleo ya taifa kupitia ulipaji wa kodi kwa hiari, akibainisha kuwa ongezeko la mapato ya serikali limewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. 

Alieleza kuwa TRA imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, ambapo makusanyo yameongezeka kutoka takribani shilingi bilioni 531 hadi matarajio ya kufikia zaidi ya shilingi trilioni 36 katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, alimpongeza Kamishna Mkuu wa TRA pamoja na watumishi wa mamlaka hiyo kwa kuboresha utoaji wa huduma, kupunguza urasimu na kujenga mahusiano mazuri na walipakodi, hatua alizosema zimeongeza imani ya wananchi kwa taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa,Maigloria Saria alisema maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo yanaambatana na shughuli mbalimbali za kurejesha kwa jamii, ikiwemo kutembelea wagonjwa hospitalini, kupanda miti na kuwashukuru walipakodi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano kati ya TRA na wananchi.

Alisema TRA imeendelea kuboresha matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma, jambo lililorahisisha ulipaji wa kodi na kuongeza uwazi pamoja na uwajibikaji.

 Aliongeza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kupanua wigo wa kodi, kuboresha huduma kwa walipakodi na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari ili kuongeza mchango katika maendeleo ya taifa.

Saria aliwataka walipakodi kuhakikisha wanalipa kodi kwa wakati, kudai na kutoa risiti halali katika kila muamala wa biashara, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni msingi wa ukusanyaji sahihi wa mapato ya serikali na maendeleo endelevu ya nchi.