Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ufadhili wa Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi ya Kijani (GCF) kwa kushirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), imefikia hatua muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa Kujenga Uhimilivu dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Mkoa wa Kigoma kwa kuanza uthibitishaji wa matokeo ya tathmini ya awali ya mradi huo.
Uthibitishaji huo unafanyika kupitia warsha iliyofanyika katika Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma Juni 26, 2026 ukilenga kuhakiki hali halisi ya kijamii, kiuchumi na kimazingira katika maeneo ya mradi kabla ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kuimarisha uhimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Meneja wa Mradi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Onesphory Kamukuru alisema mradi unatekelezwa katika wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko kutokana na maeneo hayo kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na uharibifu wa mazingira, mmomonyoko wa ardhi na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi.
Alieleza kuwa mojawapo ya sababu zilizochangia uharibifu huo ni historia ya maeneo hayo kupokea idadi kubwa ya wakimbizi, hali iliyosababisha ongezeko la matumizi ya rasilimali za misitu, ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
“Mradi huu ni wa wananchi na unatekelezwa katika maeneo matatu makuu ambayo ni kilimo mseto, usimamizi wa hifadhi za misitu ya vijiji na za TFS pamoja na kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na mmomonyoko wa ardhi,” alisema Mhandisi Kamukuru.
Mradi huo unatekelezwa katika vijiji 22 vya wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko, ambavyo vimeathiriwa kwa kiwango kikubwa na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, hususan vijiji vilivyo karibu na maeneo yaliyowahi kuhifadhi wakimbizi.
Katika mradi huu, TAFORI imepewa jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa za awali zitakazotumika kama msingi wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mradi. Aidha, taasisi hiyo inasimamia utekelezaji wa shughuli za kitaalamu katika maeneo matatu ya kipaumbele ambayo ni Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (CBFM), Kilimo Mseto (Agroforestry) na Upandaji Miti (Afforestation).
Akizungumza kwa niaba ya timu ya wataalamu wa TAFORI, Mtafiti Mwandamizi na Msimamizi wa Ushauri wa Kitaalamu wa Mradi, Dkt. Numan Amanzi, alisema matokeo ya tathmini ya awali yaliyowasilishwa kwa wadau yameridhisha na yanaakisi hali halisi iliyopo katika vijiji vinavyotekeleza mradi.
“Matokeo haya yatatumika kama msingi wa kupima mafanikio ya mradi baada ya kukamilika ili kubaini kwa kiwango gani umechangia kuboresha hali za kiuchumi, kijamii na kimazingira katika jamii husika,” alisema Dkt. Amanzi.
Hatua ya uthibitishaji wa matokeo ya tathmini ya awali ni awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi. Awamu ya kwanza ilihusisha utambulisho wa mradi kwa mamlaka za Mkoa wa Kigoma na wilaya husika, huku awamu ya pili ikihusisha uthibitishaji wa vigezo vya uteuzi wa vijiji, maeneo ya utekelezaji na aina za miti zitakazotumika katika shughuli za usimamizi shirikishi wa misitu, kilimo mseto na upandaji miti.
Warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Maafisa Mazingira, Maafisa Mkoa, Wilaya, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Wawakilishi wa vijiji 22 vya wilaya za Kasulu, kibondo na Kakonko.

