Na John Bukuku Ukonga
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuangalia uwezekano wa kuruhusu vyombo vya dola kuwekeza katika huduma ya mabasi ya mwendokasi, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi ya 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 iliyofanyika katika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam.
Alisema Mkoa wa Dar es Salaam una magereza manne pamoja na kambi mbili za magereza, huku zaidi ya wahalifu 2,000 wakiwa wamehifadhiwa katika magereza hayo, hali inayodhihirisha ukubwa wa jukumu la vyombo vya dola katika kuhakikisha usalama wa wananchi.
Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuviimarisha vyombo vya dola kupitia maboresho ya miundombinu na usafiri, akibainisha kuwa kwa miaka mingi vyombo hivyo vilikuwa vikikabiliwa na changamoto ya magari chakavu tofauti na ilivyo sasa ambapo magari yanayotumika yana ubora mkubwa.
“Leo hii magari ya vyombo vya dola yanapita barabarani yakiwa katika hali nzuri na ya kuvutia. Hii ni ishara ya namna ambavyo serikali yako imeendelea kuvijengea uwezo vyombo hivi muhimu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alisema ujenzi wa barabara mpya za kisasa jijini Dar es Salaam umeendelea kupunguza changamoto za msongamano wa magari, akitolea mfano barabara inayotoka Ikulu hadi Ukonga ambayo imejengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 231.
Alisema barabara hiyo inatarajiwa kuanza kutumika kwa huduma ya mabasi ya mwendokasi, na kupendekeza kuwa vyombo vya dola kama Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi pamoja na JWTZ vipewe nafasi ya kushiriki katika utoaji wa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, hatua hiyo itasaidia wananchi kuyaona vyombo vya dola kama sehemu ya jamii na si taasisi za kuogopwa pekee.
“Wananchi wakiona basi la magereza, polisi au jeshi wakipanda kwa huduma za kawaida za usafiri wataendelea kujenga ukaribu, kuheshimiana na kushirikiana zaidi na vyombo vya dola,” alisema.
Pia aliwataka viongozi wa kisiasa na wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga Dar es Salaam, akimpongeza Mbunge wa Ukonga kwa ushirikiano wake katika kusukuma maendeleo bila kujali tofauti za kisiasa.
