Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma Stewart Nombo,akifungua kikao cha baraza la madiwani katika ukumbi wa Halmashauri hiyo jana,kushoto Mkuu wa wilaya ya Nyasa Peres Magiri.

Baadhi ya wakuu wa idara ya Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani  Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Peres Magiri,wakati wa kikao maalum cha baraza la madiwani kilichofanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma Khalid Halif,akitoa taarifa ya mapato na matumizi kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika jana  katika ukumbi wa Halmashauri hiyo eneo la Kilosa,kulia mwakilishi wa akatibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Amandus Chilummba.

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Halif(hayupo pichani)wakati wa kikao cha  kupokea taarifa ya robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2025/2026  ambapo Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh.bilioni 2.7 kutoka mapato ya ndani.

Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Peres Magiri,akitoa salamu za Serikali  kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya Nyasa jana.

………..

Na Mwandishi Wetu, Nyasa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma, imefanikiwa kukusanya Shilingi bilioni 2.7 sawa na asilimia 85 ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 3.2 kupitia mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha utakaoishia mwezi  tarehe 30 Juni 2025/2026.

Mafanikio hayo yamepatikana huku ikiwa bado miezi miwili kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha, hali inayoonesha kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali za Halmashauri hiyo.

Akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya Halmashauri ya wilaya Nyasa katika kikao cha robo ya tatu Julai 2025 hadi Machi 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Khalid Khalif alisema,mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya viongozi, watendaji na wananchi katika kuhakikisha mapato ya ndani yanaongezeka.

Khalid alisema,Halmashauri imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo inatarajia kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 3.8, sawa na ongezeko la asilimia 17 kutoka makusanyo ya mwaka huu wa fedha.

Ameeleza kuwa Halmashauri, itaendelea kuimarisha kilimo cha zao la kokoa katika ukanda wa Ziwa Nyasa pamoja na zao la kahawa katika maeneo ya milimani, mazao ambayo yanatarajiwa kuongeza mapato ya wananchi na Halmashauri kwa ujumla.

Aidha alimesema, kupitia wakala wa mazao mchanganyiko (COPRA), Halmashauri inatarajia kupata miche kati ya elfu 50 hadi  100,000 ya kakao  kwa ajili ya kugawiwa kwa wananchi, sambamba na ununuzi wa zaidi ya miche milioni  1,000,000 ya kahawa aina ya arabica ili kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ya kimkakati.

Akitoa salamu za Serikali mkuu wa wilaya ya Nyasa Peres Magiri,amewapongeza watumishi na madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kazi kubwa ya kuibua vyanzo vipya na usimamizi mzuri wa mapato ya ndani katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026.

“Wakati  nakuja Nyasa makusanyo ya ndani yalikuwa Shilingi bilioni 2.4,leo tunazungumzia zaidi ya Sh.bilioni 3 kwa hiyo nawapongeza sana kwa kazi mnayofanya katika ukusanyaji wa mapato ya ndani,nawaomba sana endeleeni na mkakati wa kukusanya zaidi ili tuweze kufika malengo tunayopewa na Serikali,madiwani muwe sehemu ya mafanikio haya  katika Halmasauri  badala ya kuwa watazamaji”alisema Magiri.

Magiri amewataka madiwani, kwenda kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye kata zao pamoja na kuhamasisha wananchi kushikiri kikamilifu kwenye ujenzi wa miradi hiyo inayolenga kusogeza huduma na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Stewart Nombo, amewataka wataalamu wa ukusanyaji wa mapato kuendelea kusimamia kikamilifu ukusanyaji huo ili Halmashauri iweze kufikia lengo la asilimia 100 kabla ya kuhitimishwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Kwa upande wake mwakilishi wa katibu tawala  wa mkoa wa Ruvuma Amandusi Chilumba,amewataka madiwani na watumishi kuwa wamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepuka mgawanyiko unaoweza kurudisha nyuma maendeleo ya Halmashauri na wilaya ya Nyasa kwa ujumla.

Chilumba alisema,umoja na jambo la msingi kwani hata hati chafu au hati zenye mashaka inazopata Halmashauri nyingi hapa nchini chanzo chake ni migogoro ya mara kwa mara kati ya madiwani na watumishi kwani  inapotokea migogoro hawataweza kusimamia miradi ya maendeleo,mapato,fedha na mali za Serikali.