Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Biashara (Joint Trade Committee – JTC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia yamekamilika kufuatia kuhitimishwa kwa kikao cha Kamati ya Pamoja ngazi ya Makatibu Wakuu kilichofanyika leo, Mei 6, 2026, katika Kituo cha Huduma cha Pamoja Mpakani (OSBP) mjini Tunduma.

Kikao hicho cha Makatibu Wakuu ni hatua ya mwisho ya maandalizi kuelekea Mkutano wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika Mei 7, 2026, ukilenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa uchumi, biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili jirani.

Katika kikao hicho, Makatibu Wakuu walipokea, kujadili na kupitisha mapendekezo pamoja na ajenda mbalimbali zilizowasilishwa na Mkutano wa Ngazi ya Wataalamu uliofanyika Mei 4 hadi 5, 2026.

 Ajenda hizo zitawasilishwa kwa Mawaziri kwa ajili ya kutolewa maamuzi na maelekezo kwa utekelezaji wake.

Mkutano huo wa JTC unalenga kupitia maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita, kujadili changamoto mpya zinazojitokeza katika biashara mpakani, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ili kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na Zambia.

Zambia ni miongoni mwa washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania katika ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC), huku thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ikiendelea kuongezeka kutokana na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo, matumizi ya miundombinu ya kimkakati ikiwemo Reli ya TAZARA, Bandari ya Dar es Salaam pamoja na barabara ya Kimataifa ya TANZAM inayounganisha nchi hizo mbili.

Aidha, mpaka wa Tunduma na Nakonde umeeendelea kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi za SADC, ambapo mamia ya malori ya mizigo hupita kila siku yakisafirisha bidhaa mbalimbali kwenda na kutoka katika nchi za ukanda huo, hali inayoifanya Tanzania kuwa kiunganishi muhimu cha biashara na usafirishaji kwa nchi zisizo na bandari katika eneo la Kusini mwa Afrika.

Ujumbe wa Tanzani katika Mkutano huo umejumuisha Naibu Katibu Mkuu Kilimo Prof. Peter L. M. Msoffe, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mikakati na Siasa za Ulimwengu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Thobias Makoba akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Viongozi Waandamizi wa Taasisi mbalimbali za Serikali na Wadau kutoka sekta binafsi ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Aristides Mbwasi.