NA DENIS MLOWE IRINGA
KATIKA kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Fabian Ngajilo, alihoji serikali kuhusu maendeleo ya huduma za kibingwa hususan matibabu ya saratani na moyo katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Akijibu maswali ya mbunge huyo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alisema serikali inaendelea kuimarisha huduma za ubingwa katika hospitali za rufaa za mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Songwe pamoja na Hospitali ya Kanda ya Mbeya, ambayo tayari inatoa huduma za kibingwa katika maeneo ya moyo, saratani, mapafu, figo, ini na upasuaji mbalimbali.
Dkt. Samizi alibainisha kuwa ujenzi wa kituo kipya cha huduma za saratani mkoani Mbeya unaendelea, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu. Alisema jengo hilo, litakalogharimu takribani shilingi bilioni 11, litakuwa sehemu ya Taasisi ya Saratani Ocean Road na kuanza kutoa huduma za mionzi mara tu vifaa vitakapofungwa.
Mbunge Ngajilo aliomba serikali kuharakisha kuleta mtambo wa mionzi ili kupunguza adha kwa wagonjwa wanaotegemea huduma za dawa (chemotherapy) pekee kwa sasa. Aidha, alitaka ufafanuzi kuhusu utaratibu wa msamaha wa gharama za matibabu kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.
Katika majibu yake, Naibu Waziri Samizi alieleza kuwa serikali inaendelea kugharamia matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo kupitia utaratibu wa msamaha. Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 34 kwa ajili ya kugharamia matibabu ya kundi hilo. Alisema maafisa maendeleo ya jamii katika hospitali ndio wanaoratibu utambulisho na usimamizi wa wagonjwa wanaostahili msamaha huo.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, serikali itaendelea kuwekeza katika huduma za kibingwa ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora karibu na maeneo yao bila kulazimika kusafiri hadi Dar es Salaam.

