NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameagiza Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) kuongeza kasi ya utengenezaji wa mifumo ya kidigitali inayozingatia vipaumbele vya Serikali, huku akisisitiza marekebisho ya haraka ya mifumo yenye kasoro ili isikwamishe juhudi za mageuzi ya kiuchumi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga, alipomwakilisha Rais Dk. Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa mifumo miwili ya kidigitali ambayo ni Mfumo wa Malipo ya Pensheni kwa Wazee (PBMS) na Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Vivutio vya Utalii (Za Explore), iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Airport Zanzibar.
Dk. Mwinyi alisema Serikali imejipanga kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanakuwa mhimili mkuu wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kudhibiti matumizi ya fedha za umma na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.
Alisema mifumo hiyo ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidigitali unaokwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani.
Alihimiza taasisi zote za umma kuhakikisha zinatoa ushirikiano wa kutosha kwa eGAZ na kuacha tabia ya kutengeneza mifumo kienyeji bila uratibu wa mamlaka husika.
“Ni marufuku kwa wizara au taasisi yoyote kutengeneza mfumo wake bila kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao. Tumeshuhudia baadhi ya mifumo kuwa chanzo cha urasimu na upotevu wa mapato kutokana na kasoro za kiufundi,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo watendaji wa TEHAMA kupitia mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kwenda sambamba na kasi ya teknolojia mpya.
“Tusibane watendaji wetu kwenda kuongeza ujuzi. Kila ofisa wa TEHAMA anapaswa kupata nafasi ya kujifunza na kujiendeleza,” alieleza.
Rais Dk. Mwinyi pia alionya kuhusu hujuma na matumizi mabaya ya mifumo, ikiwemo baadhi ya watendaji kulazimisha matumizi ya fedha taslimu badala ya mifumo ya kielektroniki kwa maslahi binafsi.
Aliwataka makatibu wakuu na wakuu wa taasisi kuhakikisha mifumo inatumika ipasavyo na kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuimarisha vitengo vya TEHAMA.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Fatma Mabrouk, alisema Serikali inaendelea kuunganisha taasisi za umma kidigitali ili wananchi wapate huduma kwa haraka, uwazi na ufanisi zaidi.
Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika safari ya mageuzi ya kidigitali nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa eGAZ, Dk. Said Seif Said, alisema mifumo hiyo inalenga kuongeza uwazi, kurahisisha huduma na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Akizungumzia mfumo wa Za Explore, alisema mfumo huo utaunganisha vivutio mbalimbali vya utalii katika jukwaa moja litakalowezesha watalii kufanya malipo kabla ya kufika katika maeneo husika, hatua itakayorahisisha huduma na kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Alisema mfumo huo pia utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kupunguza mianya ya upotevu wa fedha.
Kuhusu Mfumo wa Malipo ya Pensheni kwa Wazee (PBMS), alisema utasaidia kuhifadhi taarifa za wazee wenye sifa na kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa wakati bila usumbufu.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Shigeki Komatsubara, alisema uzinduzi wa mfumo wa malipo bila fedha taslimu kwa maeneo ya hifadhi ni hatua kubwa ya kuimarisha uwazi na kuongeza mapato katika sekta ya utalii na uhifadhi.
Alisema mfumo huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Ufadhili wa Bioanuai (BIOFIN), unaolenga kusaidia Serikali kuimarisha usimamizi wa fedha kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa rasilimali za asili.
Kwa mujibu wa UNDP, maboresho yaliyofanywa kupitia mpango huo yanatarajiwa kuongeza mapato ya kila mwaka kutoka dola milioni 1.3 hadi dola milioni 4.3 za Marekani.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itaongeza manufaa kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi huku ikiimarisha uchumi wa buluu na kijani kupitia ajira, mapato ya ndani na utalii endelevu.
Uzinduzi wa mifumo hiyo umeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuharakisha mageuzi ya kidigitali na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha huduma za kisasa za kidigitali katika ukanda wa Afrika Mashariki.

