Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni, Dodoma 

Wizara ya Maji imesema katika mwaka wa fedha 2026/27 itaendelea kuweka mkazo kwenye utekelezaji wa miradi ya maji vijijini na mijini ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi nchini.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2026/27, Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso amesema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji sambamba na kuongeza huduma za majisafi na usafi wa mazingira.

Amesema kuwa vipaumbele vya Wizara hiyo vitajikita katika usimamizi wa rasilimali za maji, huduma za ubora wa maji, usambazaji wa maji vijijini na mijini pamoja na kudhibiti upotevu wa maji.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya maji ikiwemo mabwawa ya kuhifadhi maji, miradi ya uvunaji wa maji ya mvua pamoja na ulinzi wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama dhidi ya changamoto ya uhaba wa maji.

Pia amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za maji vijijini kupitia RUWASA kwa kukamilisha miradi mbalimbali inayoendelea katika maeneo tofauti nchini.

Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wa vijijini wanaendelea kupata huduma ya maji kwa kiwango kikubwa zaidi huku huduma za maji mijini nazo zikiendelea kuboreshwa kupitia mamlaka za maji.

Aidha, amebainisha kuwa Wizara itaendelea kudhibiti upotevu wa maji katika mifumo ya usambazaji ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha.

Pia amesema kuwa Serikali itaendelea kujenga uwezo wa kitaasisi kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA, maabara za ubora wa maji pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa sekta ya maji nchini.

Ameongeza kuwa katika mwaka 2026/27 Wizara itaendelea kusimamia ubora wa maji yanayosambazwa kwa wananchi ili kuhakikisha yanakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa kwa matumizi ya binadamu.

Vilevile, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za usafi wa mazingira mijini na vijijini kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya majitaka pamoja na kuhamasisha matumizi ya vyoo bora.

Aidha, amebainisha kuwa utekelezaji wa vipaumbele hivyo unalenga kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi ifikapo mwaka 2030.