Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

6/5/2026 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuimarisha huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo kupitia ushirikiano wa kimataifa unaolenga kubadilishana uzoefu na ujuzi na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali yaliyobobea katika utoaji wa huduma hizo.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya wakati akizungumza na madaktari bingwa wa moyo kutoka nchini Misri waliotembelea JKCI kwa engo la kujionea namna huduma zinavyotolewa na kuweka mikakati ya ushirikiano katika utoaji wa huduma za kibingwa na bobezi za matibabu ya moyo.

Dkt. Angela alisema ujio wa madaktari hao utaongeza jitihada za taasisi hiyo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora na za kibobezi kwa wagonjwa wa moyo.

“Tumewapokea madaktari wawili kutoka nchini Misri ambao watafanya upasuaji kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu, madaktari hawa wamekuja na vifaa tiba vitakavyotumika katika utoaji wa huduma”, alisema Dkt. Angela.

Aliongeza kuwa mbali na kutoa matibabu ujio huo pia utatoa fursa kwa wataalamu wa JKCI kubadilishana uzoefu na ujuzi pamoja na kuandaa mkakati wa ushirikiano wa muda mrefu utakaowezesha wataalamu hao kutembelea taasisi hiyo mara kwa mara.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kutoka Chuo cha Ain Shams kilichopo nchini Misri Prof. Atef Abdel Hameed, alisema ujio wao JKCI utasaidia kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo.

“Tumefurahi kuja JKCI kushirikiana na kubadilishana ujuzi katika masuala ya magonjwa ya moyo na upasuaji pamoja na kujifunza mbinu bora za tiba na matumizi ya dawa katika matibabu ya magonjwa ya moyo”, alisema Prof. Hameed.