Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Serikali imesema utekelezaji wa mradi mkubwa wa Bwawa la Kidunda unaolenga kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani umefikia asilimia 47.02 hadi Aprili 2026.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso, wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maji , Waziri Aweso amesema kuwa mradi huo ni mkakati muhimu wa Serikali wa kuhakikisha Mto Ruvu unaendelea kuwa na maji ya kutosha mwaka mzima kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Amesema kuwa bwawa hilo litasaidia kupunguza changamoto ya ukame ambayo imekuwa ikiathiri huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na maeneo jirani.
“Bwawa la Kidunda ni mkakati wa kuboresha ikolojia ya Mto Ruvu ili kuhakikisha maji yanapatikana kipindi chote cha mwaka,” amesema Waziri Aweso.
Mradi huo unagharimu Shilingi bilioni 329.47 na unahusisha ujenzi wa bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo milioni 190 za maji.
Pia unahusisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa megawati 20, njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 101 kutoka Kidunda hadi Chalinze pamoja na barabara ya changarawe yenye urefu wa kilomita 75.
Aweso amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa suluhisho la muda mrefu la changamoto ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ambalo limekuwa likikua kwa kasi ya idadi ya watu na shughuli za kiuchumi.
Mbali na Dar es Salaam, mradi huo pia unatarajiwa kunufaisha maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji wakati wa kiangazi.
