Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha hali ya usalama wa chakula nchini baada ya uzalishaji wa mazao ya chakula kuongezeka katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025.
Ameyasema hayo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani 23,783,128 ikilinganishwa na tani 22,803,316 za msimu wa mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.3.
Pia amesema kuwa uzalishaji huo umewezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 130 huku kukiwa na ziada ya tani 5,504,074 za chakula.
Ameongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya nafaka ulifikia tani 14,924,582 huku mazao yasiyo ya nafaka yakifikia tani 8,858,546 katika msimu wa mwaka 2024/2025.
Aidha, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha uzalishaji wa chakula kupitia uwekezaji katika mbegu bora, mbolea, umwagiliaji na huduma za ugani kwa wakulima nchini.
Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa salama kwa chakula na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa nchi.




