Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.
Ameyasema hayo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeendelea kutekeleza jumla ya miradi 780 ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia amesema kuwa miradi 28 yenye uwezo wa kumwagilia hekta 23,528 imekamilika huku miradi 118 yenye uwezo wa kumwagilia hekta 232,658 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Ameongeza kuwa Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi 189 ya umwagiliaji huku miradi 445 ikiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi.
Aidha, amesema kuwa uwekezaji huo unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza kipato cha wakulima.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya umwagiliaji ili kuhakikisha kilimo kinakuwa cha uhakika na chenye tija kwa wakulima nchini.




