Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema kuwa jitihada za Serikali katika kuimarisha diplomasia ya uchumi zimeendelea kuongeza masoko ya mazao ya kilimo nje ya nchi.
Ameyasema hayo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aidha, amebainisha kuwa thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi imeongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 3.73 mwaka 2024/2025.
Pia amesema kuwa Serikali imeendelea kufungua masoko katika nchi za Asia, Ulaya, Amerika na Afrika kwa ajili ya mazao yanayozalishwa nchini.
Ameongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka hadi tani 1,596,311.18 mwaka 2024/2025 kutoka tani 973,436 mwaka 2021/2022.
Aidha, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ubora wa mazao, kuongeza uzalishaji na kuwezesha wakulima kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.
Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza fedha za kigeni, kukuza uchumi wa Taifa na kuongeza kipato cha wakulima nchini.




