Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa Serikali inaendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuifanya sekta ya madini kuwa injini muhimu ya kukuza uchumi wa Taifa kwa kuwekeza zaidi katika mnyororo wa thamani wa madini mkakati na kuhamasisha uwekezaji katika uongezaji thamani.
Ameyabainisha hayo Aprili 27, 2026 Jijini Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, amesema kuwa madini mkakati yakiwemo lithium, graphite, nickel, cobalt na rare earth elements yana nafasi kubwa katika maendeleo ya teknolojia za kisasa hususan nishati safi. Aidha amebainisha kuwa mwelekeo wa dunia kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira unaongeza mahitaji na thamani ya madini hayo katika soko la kimataifa.
Pia ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha uwekezaji katika utafutaji na uchimbaji wa madini hayo ili kuongeza uzalishaji pamoja na mapato ya Taifa. Amesema kuwa tafiti za masoko mapya zitafanyika ili kupanua wigo wa biashara huku taratibu za utoaji leseni zikirahisishwa kwa wawekezaji.
Amesema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja kupitia ajira, mapato na maendeleo ya viwanda vinavyotokana na rasilimali hizo.
Aidha amebainisha kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji na usafishaji wa madini ili kuongeza thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi. Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza usafirishaji wa madini ghafi na kuongeza mapato kupitia bidhaa zilizoboreshwa.
Pia ameongeza kuwa eneo la Buzwagi wilayani Kahama limetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini, hatua inayotarajiwa kuvutia wawekezaji na kuongeza ajira kwa wananchi.
Aidha amebainisha kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha viwanda vya usafishaji wa dhahabu vinapata ithibati ya kimataifa ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.
Amesema kuwa Tanzania inatarajia kuandaa mkutano wa saba wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini utakaofanyika Dar es Salaam mwezi Novemba 2026, ambapo wadau mbalimbali watakutana kujadili fursa na changamoto za sekta hiyo.
Kwa upande wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/2026, amesema kuwa Wizara imepiga hatua kubwa ikiwemo kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato na kuimarisha usimamizi wa rasilimali madini.
Aidha amebainisha kuwa Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 224.98 kwa ajili ya Wizara, ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 100.38 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 124.60 kwa miradi ya maendeleo. Amesema kuwa hadi Machi 2026, Wizara ilikuwa imepokea shilingi bilioni 82.90.
Pia ameongeza kuwa katika ukusanyaji wa maduhuli, Wizara ilipangiwa kukusanya shilingi trilioni 1.41 lakini hadi Machi 2026 tayari ilikuwa imekusanya shilingi trilioni 1.03, sawa na asilimia 114.94 ya lengo la kipindi husika.
Amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na kuimarishwa kwa ukaguzi katika maeneo ya uchimbaji, masoko ya madini, vituo vya ununuzi pamoja na mipaka ya nchi ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Aidha amebainisha kuwa thamani ya biashara ya madini imeongezeka na kufikia shilingi trilioni 4.90 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026 ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.82 kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Pia ameongeza kuwa Serikali imeendelea kudhibiti utoroshaji wa madini ambapo madini yenye thamani ya shilingi bilioni 3.31 yalikamatwa katika matukio 55 na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema kuwa mapato ya fedha za kigeni yameongezeka ambapo mauzo ya madini nje ya nchi yalifikia dola milioni 5,401.9 mwaka 2025 kutoka dola milioni 4,119.9 mwaka 2024.
Aidha amebainisha kuwa mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024 na kufikia wastani wa asilimia 11.9 katika robo tatu za mwaka 2025.




