Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Wizara ya Madini imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 174.98 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, amesema kuwa fedha hizo zitawezesha wizara pamoja na taasisi zake kusimamia sekta ya madini kwa ufanisi na kufikia lengo la ukusanyaji wa maduhuli ya zaidi ya shilingi trilioni 1.4.
Amesema kuwa kati ya fedha zilizoombwa, shilingi bilioni 71.51 sawa na asilimia 40.87 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, inayolenga kukuza sekta ya madini na kuongeza thamani ya rasilimali zake.
Aidha, amebainisha kuwa shilingi bilioni 103.47 sawa na asilimia 59.13 ya bajeti yote zimeelekezwa kwenye matumizi ya kawaida, ikiwa ni pamoja na kugharamia shughuli za uendeshaji wa wizara na taasisi zake.
Pia ameongeza kuwa ndani ya matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 27.36 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi huku shilingi bilioni 76.11 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo ya kiutendaji.
Amesema kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo utawezesha kufikiwa kwa lengo la kukusanya maduhuli ya shilingi trilioni 1.406 pamoja na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali madini.
Aidha, amebainisha kuwa wizara itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.
Pia ameongeza kuwa kupitishwa kwa bajeti hiyo kutachochea ukuaji wa sekta ya madini, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuimarisha mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni.
Pia, ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha fedha zitakazoidhinishwa zinatumika kwa ufanisi na uwajibikaji mkubwa kwa manufaa ya Taifa.




