Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MWENGE wa Uhuru umeridhishwa na utekelezaji wa miradi yote 68 yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 263.1 mkoani Pwani, ukibainisha kuwa hakuna mradi wenye dosari.
Mwenge huo umepitia wilaya saba zenye halmashauri tisa katika mkoa huo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amepongeza mkoa wa Pwani kwa usimamizi mzuri wa miradi, akieleza kuwa mwaka huu wananchi wengi, wakiwemo wazee, wamefanikiwa kuuona Mwenge wa Uhuru katika maeneo ya ndani kwa mara ya kwanza, huku wengine wakidai hawajauona kwa miaka mingi.
Amesema mikoa na halmashauri nyingine zinapaswa kuiga mfano wa Pwani kwa kuhakikisha miradi inaelekezwa katika maeneo yatakayowezesha Mwenge kufika kwa wananchi wengi zaidi.
“Tumefika Ndundutawa, Kata ya Shela, wananchi wanasema hawajawahi kuuona Mwenge kwa miaka mingi.
” Tunapongeza Pwani kwa kazi hiyo nzuri na tunaomba mikoa na halmashauri nyingine ziige mfano huu ili wananchi waweze kuushuhudia Mwenge wao,” alieleza Mwang’onda.
Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akikabidhi Mwenge wa Uhuru mpakani mwa mkoa wa Pwani na Lindi katika eneo la Somanga Aprili 27, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alishukuru na kueleza kuwa miradi yote 68 iliyopitiwa haina dosari, huku akiahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.
Alifafanua kuwa kati ya miradi hiyo, miradi 23 imewekewa mawe ya msingi, 17 imezinduliwa na 24 imekaguliwa.
Mwenge wa Uhuru 2026 unabeba ujumbe wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa chini ya kaulimbiu isemayo: “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”





