Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Zacharia Kafulila, amesema kuwa Muungano wa Tanzania ni wa kipekee barani Afrika kwa kuwa umejengwa juu ya umoja wa watu badala ya serikali pekee.
Kafulila ametoa kauli hiyo katika maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano, akieleza kuwa huu ndio Muungano pekee wa mataifa mawili huru uliodumu kwa zaidi ya miongo sita bila kuvunjika, tofauti na miungano mingine iliyoshindwa kudumu kwa muda mfupi.
Ametolea mfano miungano iliyovunjika ikiwemo ya Ethiopia na Eritrea (1952–1962), pamoja na Muungano wa Ghana, Guinea na Mali (1958–1963), na ule wa Senegambia (1982–1989) ambao haukudumu.
Kwa mujibu wa Kafulila, siri ya mafanikio ya Muungano wa Tanzania ni asili yake ya udugu na utamaduni, ambapo umejengwa juu ya misingi ya lugha ya Kiswahili, historia ya pamoja na mshikamano wa kijamii.
Ameongeza kuwa tofauti na miungano mingine ya Ulaya na Asia inayotegemea zaidi makubaliano ya kiuchumi na kibiashara, Muungano wa Tanzania una nguvu ya kipekee ya “umoja wa watu”.
Aidha, amesisitiza kuwa Watanzania wataendelea kuenzi mchango wa waasisi wa Muungano huo, Julius Nyerere na Abeid Karume, kwa kuweka misingi imara iliyowezesha kudumu kwa Muungano huo hadi leo.




