Na Mwamvua Mwinyi, Kibiti
JUMLA ya miradi nane yenye thamani ya shilingi bilioni 3.916 imepitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Kibiti, mkoani Pwani, huku miradi miwili ikizinduliwa, mitatu kukaguliwa na mingine mitatu kuwekwa mawe ya msingi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo, wakati akipokea Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Shule ya Msingi Ujamaa, kata ya Mjawa, ukitokea wilayani Mkuranga.
Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa maji ya bomba katika kijiji cha Mlanzi unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa mwaka wa fedha 2023/2024, unaotarajiwa kunufaisha wananchi takribani 6,095.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa RUWASA wilayani Kibiti, Ramadhan Mabula, amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi M/S Frederick Construction Company Limited wa Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi milioni 936.46.
Amesema hadi sasa mkandarasi amelipwa zaidi ya shilingi milioni 353.8, huku utekelezaji wa mradi ukifikia asilimia 95.
Akikagua mradi huo na kuweka jiwe la msingi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
Pia ameipongeza RUWASA kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mwang’onda amewataka wananchi kutunza miradi hiyo ili iweze kudumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo, akieleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya maji.
Mradi mwingine uliopitiwa ni ujenzi wa madarasa matatu na ofisi katika Shule ya sekondari wananchi, ujenzi wa mifereji yenye urefu wa kilomita tano, kalavati 22 na vivuko, uliogharimu shilingi bilioni 1.9, kituo cha afya Bungu, zahanati ya Mwangia , Mradi wa ghala la kuhifadhia mazao, kugawa mitungi ya gesi ya kupikia kwa mama lishe na kuzindua Mradi wa bus coaster la vijana UWAKITE.
Mwenge wa Uhuru umefikisha siku ya nane mkoani Pwani tangu ulipopokelewa Aprili 18, 2026, ambapo unatarajiwa kumalizia mbio zake Aprili 26, 2026 katika Halmashauri ya Rufiji kabla ya kukabidhiwa mkoani Lindi Aprili 27, 2026.






